VITA vya ubunge mkoani Kilimanjaro vimepamba moto ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya makada 124 kuonyesha nia ya kuomba uteuzi wa kugombea nafasi hiyo katika majimbo tisa ya mkoa huo.
Mchakato huo unatokana na wabunge wote nchini, kumaliza muda wao wa uongozi kwa kipindi cha miaka mitano, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, alisema hadi kufikia Jumatatu, ofisi yake ilikuwa imepokea jumla ya wanachama 124 wanaoomba nafasi hiyo.
“Tangu ilipotoka kauli rasmi ya kiongozi wetu ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi ngazi ya taifa, na sisi kama wasaidizi wake naomba nitoe taaarifa kuhusu nmchakato unaoendelea hapa Kilimanjaro.
“Hadi kufikia Julai 6, mwaka huu, tumepokea jumla ya wanachama 124. Hawa ni wale wanaoonyesha nia yao ya kuomba uteuzi wa kugombea ubunge katika majimbo tisa ya mkoa wa Kilimanjaro.”
Alitaja majimbo na idadi ya watiania kwenye mabano kuwa ni Moshi Mjini (8), Moshi Vijijini (22), Jimbo la Vunjo (13) na Jimbo la Same Magharibi (13).
Majimbo mengine ni Same Mashariki (16), Jimbo la Hai (8), Jimbo la Siha (7), Mwanga (23) 23 na Rombo (14).
Kutokana na idadi ya watia nia kuongezeka kila uchao mkoani humo, Mabihya alisema: “Kwa mujibu wa katiba yetu na kanuni za CCM, wakurugenzi wa uchaguzi ni makatibu wa chama wa ngazi husika.
“Kwa maana ya makatibu wa mikoa, makatibu wa wilaya, makatibu kata na makatibu wa matawi, hao ndio wakurugenzi unapofika wakati wa uchaguzi. Kwa hiyo tunaposema kupitapita maana yake watu waende ofisi za chama, huenda mtu alikuwa na dhamira ya kugombea, lakini alikuwa hajui wapi pa kwenda kusema dhamira hiyo,” alisema.
“Hivyo ni wakati muafaka wa kwenda kwenye ofisi za chama ili tuweze kuwatambua.”
Juni 12 mwaka huu, CCM ilipuliza kipenga cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa kufungua dirisha la kuchukua na kurudisha fomu kwa wanaowania nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa wanaowania nafasi ya udiwani, uwakilishi na ubunge kwa Tanzania Bara na Visiwani, dirisha la kuchukua na kurudisha fomu, litafunguliwa Julai 14 hadi 17, mwaka huu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464