Mashabiki wa timu za Simba na Yanga wakishuhudia mchezo uliozikutanisha timu hizo Julai 14, 2020.
Mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC)
maarufu kama Kombe la FA uliowakutanisha watani wa jadi Simba SC na Yanga SC
zote za jijini Dar es Salaam Julai 12, 2020 katika Uwanja wa Taifa, umeingiza
jumla ya Sh Milioni 269, 100,000.
Nusu fainali hiyo ambayo ilishuhudia timu ya Simba ikitinga
hatua ya fainali baada ya kuwakung’uta watani wao kwa mabao 4-1, uliingiza
jumla ya mashabiki 22,990.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 14, 2020 na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeonyesha mchanganuo wa mauzo ya tiketi kwa
mchezo huo, ambapo VIP A ziliuzwa tiketi 93 sawa na Sh 2,790,00 na VIP B tiketi
1,520 sawa na Sh 38,000,000.
VIP C ziliuzwa tiketi 1,454 sawa na Sh 29,080,000 na Popular
zikauzwa tiketi 19,923 sawa na Sh 199,230,000 ambapo jumla ni Sh 269,100,000.
Simba itacheza fainali ya michuano hiyo dhidi ya Namungo FC
Agosti 2, 2020 katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoa wa Rukwa,
ambapo Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kombe la
shirikisho ngazi ya vilabu barani Afrika.