Naibu waziri wa Ujenzi, Eliasi Kwandikwa leo Julai 15, 2020 akirudisha fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la ushetu ili aweze kutetea kiti hicho.
Salvatory Ntandu-Kahama
Jumla ya Wanachama 99 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge katika majimbo ya Msalala, Ushetu na Kahama Mjini mkoani Shinyanga ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza zoezi la utoaji fomu za kuwania nafasi za Udiwani na Ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika mbio hizo vijana wameonekana kuhamasika kwa wingi ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 15, 2020 baada ya kukamilisha siku ya pili ya utoaji fomu hizo, Katibu wa CCM wilaya ya Kahama, Emmanuel Mbamange amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na vijana ndio kundi pekee lililotia fora katika zoezi la hilo huku wanawake 9 nao wakijitokeza kuwania nafasi za ubunge katika majimbo hayo.
Amesema kuwa katika Jimbo la Kahama Mjini mpaka sasa wamejitokeza wagombea 53 kati yao wanawake ni sita, ambapo nusu ya waliochukua fomu ni vijana hali inaonyesha kukua kwa demokrasia ndani ya CCM mpya inayowavutia vijana wengi kukipenda chama hicho.
Miongoni mwa wanachama wa CCM waliochukua fomu hii leo kusaka nafasi ya ubunge wa jimbo la Kahama Mjini ni pamoja na Msanii wa kizazi kipya, Bonta Maarifa kutoka Kundi la Hiphop la WEUSI pamoja na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Benjamini Ngayiwa.
Kwa upande wa Jimbo la Msalala, Mbamange amesema kuwa hadi sasa kuna wagombea 33 akiwemo mwanamke mmoja, huku Jimbo la Ushetu likiwa na wagombea 13 akiwemo mwanamke mmoja.
Mbamange alisema kuwa mpaka sasa Jumla ya wagombea 18 wamesharudisha fomu baada ya kumaliza kujaza, huku akisisitiza kuwa wagombea wote wanapaswa kuzisoma fomu hizo kwa umakini ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima kwani wapo baadhi wanajaza kinyume na utaratibu unaotakiwa.
“Lengo letu sio kuwakosesha pindi mnapojaza fomu zenu hakikisheni mnajaza kwa ufasaha na hata kama ikitokea umekosea kujaza usianze kunung’unika njoo ofisini tutakupatia fomu zingine ili ujaze kwa ufasaha na hii ndio demokrasia inayotakiwa ndani ya CCM mpya," alisema Mbamange.
Katika hatua nyingine Mbamange amewataka wagombea kutojihusisha na vitendo vya kampeni kabla ya muda jambo ambalo linaweza kusababisha wakakosa sifa na kuondolewa katika nafasi wanazoziomba na badala yake wazingatie maelekezo yaliyotolewa na chama katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige leo amechukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea tena ubunge wa jimbo hilo.
Msanii wa Muziki wa Hip Hop kutoka kundi la WEUSI, Bonta Maarifa akichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika jimbo la Kahama Mjini.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Benjamin Ngayiwa akipokea fomu ya kugombea ubunge katika jimbo la Kahama Mjini kutoka kwa katibu wa CCM wilaya ya Kahama, Emanuel Mbamange.
Mtendaji wa Kata ya Chela John Mahona akipokea fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa jimbo la Msalala.