Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
Katika zoezi la upigaji kura za maoni kwa watia nia wa nafasi za ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lililofanyika jana Julai 2020, haya ni miongoni mwa majina ya Mawaziri, waliokuwa wakuu wa mikoa mbalimbali na wanasiasa mashuhuri waliobwagwa kwenye mchakato huo wa kupata wateuliwa watakaokiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Miongoni mwao ni Waziri wa Habari, Utamdauni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya ndani na mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga.
Karibu Mawaziri na Manaibu waziri wote wamepita kwa kishindo katika majimbo yao, lakini kwa Dk. Harrison Mwakyembe mambo yamekwenda tofauti na kujikuta kwenye mshangao mkubwa baada ya kujikuta katika nafasi ya tatu kwenye kichang'anyiro cha Jimbo la Kyela mkoani Mbeya.
Katika uchaguzi huo, Ally Mlagila Jumbe ameshinda kwa kura 502, akifuatiwa na Hanta Albert Mwakifuna aliyepata kura 288, huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiibukia katika nafasi ya tatu kwa kura 252.
Dk. Harrison Mwakyembe
Katika Jimbo la Nkenge wilayani Missenyi mkoa wa Kagera, mtia nia Frolent Kyombo (103) aliwabwaga chini wagombea wenzake akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Assumpta Mshama aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 93 akifuatiwa na Balozi Dk Diodorous Kamala aliyeambulia kura 24.
Dk. Diodorius Kamala
Katika Jimbo la Buchosa mkaoni Mwanza, aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo na mbunge wa jimbo hilo, Dk. Charles Tizeba alifungana kura na mshindani wake wa karibu, Mkurugenzi wa Global Publishers na Global TV, Erick Shigongo, ambapo kila mmoja alipata kura 354.
Dk. Charles Tizeba
Jimboni Makete, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Prof. Norman Sigalla amebwagwa chini baada ya kuambulia kura 89 katika nafasi ya pili, huku mpinzani wake, Festo Sanga ambaye ni Mkurugenzi wa timu ya soka ya Singida United akiibuka kinara kwa kura 116.
Prof. Norman Sigalla
Mkoani Mwanza, katika Jimbo la Misungwi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ameibuka kinara kwa kura 406 akimbwaga aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Charles Kitwanga aliyepata kura 260.
Charles Kitwanga
Katika Jimbo la Temeke mkoani Dar es Salaam, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Mtolea naye katoka chali baada ya kuzidiwa kura na mshindi wa kura hizo, Abbas Mtemvu aliyepata kura 203, huku Mtolea akiambulia kura 22.
Abdallah Mtolea
Huko mkoani Kilimanjaro katika Jimbo la Siha, Dr. Godwin Mollel aliibuka kinara wa mchakato huo akipata kura 148 na kumshinda mshindani wake wa karibu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliyepata kura Mwanri 147 akizidiwa kura moja pekee.
Aggrey Mwanri
Katika Jimbo la Kasulu Mjini, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako aliibuka kidedea kwa kura 105 akimshinda mwanasiasa mkongwe, Daniel Nsanzugwako aliyeambulia kura 80.
Daniel Nsanzugwako
Mkoani Kilimanjaro wanasiasa wakongwe wameendelea kupata upinzani baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Jumanne Maghembe kuangukia chali katika mchakato huo, ambapo mshindani wake Anania Tadayo aliibuka kinara kwa kura 176, huku Maghembe akipata kura 130.
Jumanne Maghembe
Jimboni Tunduma, Aden Mwakyonde amepata ushindi kwenye mchakato huo akipata kura 250, wakati aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David Silinde akiibukia katika nafasi ya pili kwa kura 118.
David Silinde
Mambo yalizidi kuwaduza zaidi wanasiasa wakongwe na wabunge wanaotetea majimbo yao, ambapo huko mkoani Tabora katika jimbo la Tabora Mjini, Mwanasiasa Ismail Aden Rage aliambulia nafasi ya pili baada ya kubwagwa chini na Emmanuel Mwakasaka aliyepata kura 384 dhidi ya 235 za Rage.
Ismail Aden Rage
Huko mkoani Shinyanga, katika jimbo la Shinyanga Mjini, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobasi Katambi amejikuta akishindwa hata kuingia tatu bora baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Stephen Masele kuibuka kinara kwa kura 152.
Patrobasi Katambi