Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama cha ADC Doyo Hassan, akimkabidhi fomu ya kuwania Urais Queen Sendiga.
Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimesema kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu kumekuwa na mwamko zaidi kwa upande wa wanawake ndani ya chama hicho, ambapo kati ya watia nia ya Ubunge na Udiwani 160 nchi nzima zaidi ya watia nia 40 ni wanawake.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Doyo Hassan Doyo, wakati akimkabidhi fomu ya kugombea nafasi ya Urais mtia nia wa pili kupitia chama hicho, Queen Sendiga, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuwania nafasi hiyo mwaka huu ndani ya ADC.
"Chama chetu kinazingatia usawa wa kijinsia na ni moja ya kipengele muhimu kwenye katiba yetu ya chama, mwaka huu pia mwamko ni mkubwa kwa wanawake kuwania nafasi za uongozi", amesema Doyo.
Kwa Upande wake mtia Nia huyo Queen Sendiga, amevitaja vipaumbele vyake endapo chama chake kikimpa ridhaa ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Elimu, Afya na sekta ya kilimo.
"Vipaumbele vyangu endapo chama changu kikinipatia ridhaa ya kuwania nafasi hii ya Urais mwaka huu, nitaanza na Elimu kwa kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo mishahara na makazi, ntaongeza vituo vya Afya na kusomesha wataalam wengi zaidi ili kulisaidia Taifa", amesema Bi. Sendiga.
Queen Sendiga, mtia nia wa nafasi ya Urais kupitia chama cha ADC
Queen Sendiga anakuwa mgombea wa pili wa chama hicho kwa upande wa Bara akitanguliwa na Shaban Itutu, huku upande wa Zanzibar tayari Mwenyekiti wa chama hicho Hamad Rashid ameshatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.