Ukiulizwa uelezee ni mambo gani ambayo hufanyika hospitalini, bila shaka harusi haitakua miongoni mwa mambo utakayoyataja, ila mambo yalikua tofauti kwa wapenzi hawa wa Burundi.Charlotte Mukantwari na Gabin Ndayizigiye ni wakazi wa wilaya ya Kirundo Kaskazini mwa Burundi, kwao hakuna jambo ambalo lingewazuia kufunga pingu za maisha hata kama ni hospitalini.
Baada ya bwana harusi mtarajiwa Gabin kupata ajali mwanzoni mwa wiki iliyopita ambapo walikua wamepanga harusi yao ifanyike, alijiuliza mengi.
"Baada ya kupata ajali… niliwaza kwamba: 'Ni shetani ambaye hataki nioe?' Nilikuwa nafahamu fika kwamba siku ya tarehe nne mwezi wa saba ni siku yangu muhimu maishani,..tuliindaa pamoja nae, lazima harusi ifanyike"., aliiambia BBC.
"Tusingeoana ningehisi kama Mungu amenitupa".
Kwa upande wake bibi harusi pia anasema kuwa asingeweza kuahirisha harusi.
"Kwa jinsi nimpendavyo, kusema ukweli nilisema hata kama kuna tatizo la ajali limetokea nilihisi hakuna kitu kinachoweza kuahirisha harusi yetu ".
Wakati wa ndoa yao ya hospitalini Charlotte aliapa kumpenda mume wake Gabin daima, awe mgonjwa au mwenye afya …na wakati wa shida na raha.
Gabin nae aliapa kuishi nae wakati wa shida na raha, awe mwenye afya au awe mgonjwa.
Gabin aliiambia BBC kuwa yeye na mpenzi wake Charlotte wamekua wapenzi kwa muda mrefu na kwamba walikua wameahidi kuishi kama mume na mke hadi kifo kiwatenganishe.
Siku tatu kabla ya siku yao muhimu Gabin, aligongwa na gari na matokeo yake mguu wake ukavunjika.
"Nilipopata fahamu nilijipata nikiwa nimelala kwenye mfereji wa maji machafu, huku mguu wangu umevimba, waliokua wananiuguza waliogopa hata kumwambia Charlotte yaliyonisibu…waliogopa kumwambia kuwa niliumia sana, lakini baadae wakamwambia, akaja kuniangalia hospitalini mara moja".
Charlotte anasema kuwa alikuwa akimpigia simu mara kwa mara kumjulia hali na kumuuliza iwapo amefika nyumbani, simu ilikua inaita lakini Gabin hakuijibu.
Alipopata taarifa alijiunga na wauguzi na kumuuguza mpenzi wake, aliiambia BBC.
Gabin anasema alikuwa anadhani kwamba harusi yao huenda isifanyike, lakini alishangazwa sana na maneno ya Charlotte aliyomwambia akiwa katika kitanda cha hospitali.
" Charlotte alikuwa ananitazama kitandani, anautazama mguu wangu uliovunjika , lakini aliendelea kunipa moyo na kuniambia …''hivi tukibahatika Mungu akakupa nafuu mpango wetu wa harusi si unaweza kuendelea ?"
Aliniuliza tu hivyo tukiwa peke yetu wawili ikanishangaza sana, wakati wasichana wengine anaweza kuona umepata ulemavu hivyo anaona hapaswi hata kuwa kando yako!", anasema Gabin.
Baadae Gabin aliwasilisha pendekezo hilo kwa padre mkuu wa parokia (Paroko) yao ya Kirundo, akamuelezea kuhusu ajali aliyopata pamoja na nia yake ya kuoana na mpenzi wake Charlotte.
Padre alikubali ombi lake na akamwambia kuwa sheria za Kanisa Katoliki zinaruhusu …wanaweza kuoana hospitalini.
Basi uongozi wa hospitali uliandaa chumba ambacho wawili hao walifunga pingu zao za maisha, wakawaandalia na kiti cha wagonjwa cha magurudumu ili kumuwezesha kuondoka kitandani katika wodi alikokuwa amelazwa.
Gabin anasema ilikuwa ni kama ndoto kwake na kwa watu walio waliokua palke hospitali kushuhudia harusi yake ikifanyika katika mazingira ya hospitali.
Ingawa padre alikuwa amewaficha muda halisi wa kuwafungisha ndoa, ili kuepusha umati wa watu kuhudhuria harusi hiyo ya kipekee, hilo halikuzuwia umati wa watu kufika hospitalini kushuhudia harusi yao.
"...Sikukuu yetu ikafana, wakatupa baraka, tukavalishana pete, tukarudi tena wodini kwangu, nikaendelea kulazwa ".
Charlotte anasema siku Bwana yake Gabin atakapopona watamshukuru Mungu sana, lakini akasema hawatafanya tena harusi nyingine kwasababu hawawezi kufanya harusi mara mbili.
Lakini Bwana yake Gabin, anapanga kufanya sherehe ya kifamilia siku watakapopata mtoto na kumfanyia sherehe ya ubatizo.
Anasema: "... Tutakumbushana yote, iwe sherehe kubwa ya kupendeza na familia zote tukiwa pamoja wenye afya".
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464