NI RASMI: YANGA NA SIMBA KUKUTANA NUSU FAINALI YA FA, NAMUNGO KUVAANA NA SAHARE




Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog

USIYEMTAKA Kaja! ndivyo unavyoweza kusema, hii ni baada ya Wekundu wa Msimbazi Simba SC kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu kama Kombe la FA, ambapo sasa watakutana na watani wao wa jadi, Wana Jangwani Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali.

Sasa ni Rasmi Watani hao wa jadi watakutana kwa mara ya tatu msimu huu kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA, wakiwa tayari wamekutana kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu, mchezo wa kwanza wakitoka sare ya mabao 2-2 na mchezo wa pili Yanga wakaibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Bernard Morrison, huenda hii ikawa nafasi ya Simba SC kulipa kisasi hicho.

Simba wamefuzu hatua ya nusu fainali leo Julai 1, 2020 baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakipachikwa nyavuni na Nahodha, John Bocco na Cloutous Chama.

Katika mchezo mwingine wa robo fainali uliopigwa leo, ulizikutanisha timu za Sahare All Stars ya Tanga dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara ukipigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga, ambapo Wenyeji Sahare ambao wanatoka ligi daraja la kwanza wamefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA baada ya kuifunga Ndanda kwa Penalti 4-3 kufuatia mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sasa Sahare All Stars ambayo ni timu pekee nje ya Ligi Kuu iliyofuzu hatua ya nusu fainali, itakutana na Namungo FC ya Lindi kwenye mchezo wa nusu fainali kusaka timu itakayotinga hatua ya fainali.

Yanga walifuzu hatua hiyo baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2 -1 kwenye mchezo uliochezwa jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Namungo FC wakifuzu kwa kuikung'uta Alliance FC kwa mabao 2 -0.

Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya vilabu barani Afrika kwenye kombe la Shirikisho.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464