Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto
JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi
na usalama limejipanga kudhibiti vitendo vya utapeli kwa washiriki
uchaguzi kwa kujifanya wapo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa wakati
wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma (SAC), Gilles Muroto amesema wamejipanga kudhibiti vitendo hivyo
ili mkutano huo ufanyike kwa usalama na amani bila vitendo vya utapeli
kutamalaki.
“Jeshi limejipanga kuhakikisha yeyote atakayejaribu kufanya utapeli
wa kujifanya yupo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa hawataondoka
Dodoma, wajipange kubakia ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,”
alisema Muroto.
Katika Mkutano Mkuu wa CCM ulioanza leo Julai 7 hadi 12, mwaka huu,
utachagua na kupitisha wagombea wa nafasi ya Rais Tanzania Bara na
Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Muroto amesisitiza; “Sitataka kuona vitendo vya utapeli katika
mkutano huu unahudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa, viongozi wa
Serikali wastaafu, viongozi wa vyama rafiki wa CCM kutoka mataifa
mbalimbali duniani na kutoka katika mikoa mbalimbali.”
Muroto amesema mkutano huo unaotarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya
3,000 hatapenda kuwaona watu wanaotaka kutenda vitendo vya kitapeli kwa
kujifanya wapo karibu na viongozi.
Amesema uzoefu unaonesha kwamba katika mikutano kama hiyo wamekuwa
wakihudhuria watu mbalimbali wakiwemo wapambe wa wagombea, familia za
wagombea, wapiga debe, wajasiliamari, lakini pia wanakuwepo watu wabaya
ambao wanatumia fursa hiyo kutekeleza azma yao ya kitapeli.
Muroto amesema makundi hayo ambayo yanapanga kufanya vitendo vya
kihalifu yasije yakaingia katika mtego ambao hawakutarajia, jeshi hilo
limejiandaa kikamilifu kulinda vitendo hivyo vya kitapeli visitokee.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464