Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imetangaza kuwa Marehemu Mzee Benjamin
William Mkapa Rais Mstaafu wa awamu ya tatu atazikwa kijijini kwake Lupaso, wilaya ya
Masasi mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuanzia siku ya
Jumapili, Watanzania wote watapata fursa ya kushiriki shughuli za kuaga
zitakazofanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.
Shughuli za kumuaga mzee Mkapa zitafanyika kwa siku tatu mfululizo
kuanzia tarehe 26 mpaka tarehe 28, kuanzia Jumapili mpaka Jumanne.
Siku ya Jumapili kuanzia saa nne asubuhi, Kanisa Katoliki
litaongoza misa ambayo wakazi wa Dar es Salaam na nje ya mji huo watapata fursa
ya kuaga mwili baada ya misa na zoezi hilo litaendelea siku nzima mpaka siku ya
Jumatatu siku nzima pia itatumika kwa shughuli hiyo.
Waziri Majaliwa amesema siku ya Jumanne tarehe 28 itakuwa siku
ya kuaga kitaifa ambapo viongozi mbalimbali wa serikali nchini , viongozi wa
dini, na wananchi.
Baada ya zoezi hilo majira ya alasiri mwili wa Kiongozi mstaafu
wa taifa hilo utasafirishwa kwenda wilayani Masasi.
Mwili wa marehemu utatua katika uwanja wa ndege wa Nachingwea na
kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo kuaga mwili wa marehemu.
Waziri Majaliwa amewaambia waandishi wa habari kuwa mwili wa
marehemu utapumzishwa Siku ya Jumatano tarehe 29.
Rais mstaafu wa Serikali ya awamu ya tatu nchini Tanzania
Benjamin William Mkapa amefariki akiwa na miaka 81.
Rais John Pombe Magufuli ametangaza usiku wa kuamkia leo Ijumaa
kupitia runinga ya taifa taarifa za kufariki dunia kwa kiongozi huyo wa awamu
ya tatu katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa
matibabu.
Rais Magufuli alisema Bw. Mkapa amekuwa akipokea matibabu katika
hospitali moja jiji Dar es Salaam, na kuongeza kuwa maelezo zaidi yatatolewa
baadae.
''Mzee Benjamin William Mkapa
Rais wa awamu ya tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali mjini Dar es Salaam
ambako alikuwa amelazwa. Niwaombe watanzania tulipokee hili. Taifa limepata
msiba mkubwa. Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye
ametangulia mbele ya haki," ametangaza rais Magufuli.
@ShinyangaPressClubblog- Jukwaa la Habari Tanzania
Uhakika wa Taarifa.
#Kama Una Habari,Picha,Tukio ,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 789 632 732, +255 756 546 015 au +255 686 057 440 Email : shinyapress@gmail.com
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464