Kiungo wa timu ya Simba, Gerson Fraga akishangilia kwa kunyoosha mikono juu baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza.
Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
TIMU ya Simba SC leo imefanikiwa kusonga mbele na kutinga
fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu kama Kombe la FA, baada
ya kuwachapa watani wao wa jadi, Yanga SC kwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu
fainali uliopigwa leo saa 11 jioni katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba wameingia kwa nguvu kubwa katika mchezo huo wakihitaji
kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu Machi, mwaka
huu, ambapo wameutawala mchezo huo wakitandika kandanda safi na kupoteza
matumaini ya wapinzani wao kupata ushindi.
Mabao ya Simba yamefungwa na Gerson Fraga mnamo dakika ya 20, Cloutous Chama (50), Louis Miquissone (52) na Mzamiru Yassin (88), huku bao
la kufutia machozi la Yanga likipachikwa nyavuni na Feisal Salum ‘Fei Toto’
katika dakika ya 71.
Mchezaji wa Simba, Mzamiru Yassin akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la nne.
Kufuatia ushindi huo, Wekundu wa Msimbazi Simba watakutana
na Namungo FC ya Lindi katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo mwanzoni mwa
mwezi Agosti, 2020 katika uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga mkoani
Rukwa.
Namungo FC ambao ni msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu,
walitinga hatua ya fainali jana Julai 11, 2020 baada ya kuwanyuka Sahare All
Stars kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani
Tanga.