Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa akionyesha baadhi ya doti za khanga alizokutwa nazo mtuhumiwa.
Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
KATIKA ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa kstiks kipini hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa viongozi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga, inamshikilia Joseph Jonas Tasia kwa kukutwa na doti 600 za vitenge vyenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vya kawaida.
Tasia ambaye ni mfanyabiashara wa usafiri wa magari madogo (Taxi), alikamatwa Juni 29, mwaka huu saa 3 usiku katika mtaa wa Mwasele B akiwa nyumbani kwake, ambapo vitenge hivyo vilikamatwa vikiwa vimehifadhiwa kwake jambo ambalo linaashiria kuwa vilikuwa vinaandaliwa kutumika kufanya ushawishi kwa wapiga kura.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 3, 2020 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa imesema kuwa katika uchunguzi wake wamebaini kuwa mtuhumiwa huyo hana duka na wala hafanyi biashara ya kuuza vitenge.
“Katika mahojiano na maafisa wa Takukuru baada ya mtuhumiwa kukamatwa na mzigo huo ameshindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kuhusiana na mzigo husika na hata nyaraka za manunuzi alizowasilisha hazijitoshelezi na hivyo kuongeza mashaka juuu ya uhalali wa vitenge hivyo,” amesema Mussa.
Hussein Mussa akionyesha doti za Khanga zilizokamatwa
Mussa ameongeza kwa kueleza kuwa uchunguzi wa kina bado unaendelea ili kubaini miwapo vitenge hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya kuhusika na vitendo vya rushwa katika uchaguzi ujao au ni kwa ajili ya kufanya biashara katika msimu huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa viongozi.
“Taarifa rasmi itatolewa mara baada ya uchunguzi kufichua ukweli uliojificha, tunapenda kuwaonya watu wote wenye nia ya kutaka kutumia taarifa zozote za uchunguzi zinazofanyiwa kazi na ofisi yetu kwa nia ya kujinufaisha kisiasa na kwamba kitendo hicho ni kuingilia uchunguzi unaondelea na ni kosa la jinai, hivyo atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema.
Sehemu ya doti za khanga zilizokamatwa na Takukuru