ALIYEKUWA mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kalenge, Wilaya ya
Biharamulo mkoani Kagera, aliyefukuzwa shule kwa madai ya kuwa na
ugonjwa ambao anaweza kuwaambukiza wanafunzi wenzake, amefaulu mtihani
wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana kwa daraja la pili licha
ya kutoufanya.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Mkoa wa Kagera (Takukuru), John Joseph, jana amesema kuwa tayari
wanawashikilia walimu watatu wa shule hiyo ambao ni Mkuu wa Shule,
Boniface Eliyaabi, Makamu wake, Edwin Valentine na Edvace Richard kwa
makosa ya rushwa, hasa matumizi mabaya ya ofisi kwa kufanya usajili kwa
udanganyifu katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana.
Joseph alisema walimu hao baada ya kumfukuza shule mwanafunzi huyo,
walimuingiza shuleni mwanafunzi mwingine ambaye alitumia namba ya
mtihani ya mwanafunzi aliyefukuzwa kufanyia mtihani huo wa taifa na
kufaulu kwa daraja la pili.
“Kibaya zaidi mwanafunzi huyo ambaye aliingizwa kufanya mtihani kwa
kutumia namba ya mwanafunzi mwingine ni ndugu wa mmoja kati ya walimu
hao.
“Baada ya matokeo kutoka, mwanafunzi aliyefukuzwa aliona amepata
daraja la pili wakati huo akiwa hajafanya mtihani. Ndipo hofu ikaanza
kwa mwanafunzi huyo ambaye hakufanya mtihani jambo lililomlazimu
kushirikiana na baba yake kwenda kutoa taarifa Takukuru Juni 19, 2020,”
alisema Joseph.
Alisema kuwa walimu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya
taratibu za uchunguzi kukamilika kwa makosa ya kufanya udanganyifu
katika mitihani kwa manufaa yao kwa kumfukuza mwanafunzi shule kwa
kumsingizia kwamba ni mgonjwa na anaweza kuwaambukiza wanafunzi wengine
na kisha wakamwingiza mwanafunzi mwingine ili aweze kufanya mtihani kwa
kutumia namba yake ya mtihani.
CHANZO -MTANZANIA DIGITAL
CHANZO -MTANZANIA DIGITAL
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464