Na Mwandishi Wetu
Wakati zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa nafasi ya
Urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likifikia tamati, Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar kimefurahishwa na uthubutu wa wanawake kujitokeza kuwania nafasi hizo.
Tamwa Zanzibar imewapongeza kwa dhati
wanawake wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa wagombea wa kiti
cha Urais Zanzibar kupitia chama hicho.
Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya mgombea Urais Zanzibar
ulioanza Juni 15, mwaka huu, jumla ya wanachama 32 wamejitokeza kwenye
kinyanganyiro hicho ambapo wanachama watano (5) sawa na asilimia 15 walikuwa ni
wanawake.
Wanawake hao ni pamoja na Mwantum Mussa, Hassna Attai, Fatma
Kombo, Mgeni Hassan na Maudline Castico.
Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 1, 2020 na Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambapo amekipongeza CCM kwa kuwawezesha wanawake hao kuweza kugombea hadi katika hatua hiyo ya uongozi.
"Tunaamimi sasa wakati umefika kwa jamii wakiwemo wanasiasa kulichukulia suala hili kwa uzito unaostahiki na hivyo kuwapa nafasi wanawake kuonesha uwezo wao wa kuongoza katika nyanja mbali mbali.
Tunatamani pia CCM itachagua mmoja kati ya wanawake hao ili kuweza kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020," amesema.
Dkt. Mzuri amesema TAMWA Zanzibar inaamini kwamba ujasiri huo ulioonyeshwa na wanawake hao waliojitokeza utasaidia kuongeza hamasa zaidi kwa wanawake vijana kuendelea kujiamini na kuona kuwa wanayo nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi zote za maamuzi kwa mstakabali wa taifa lao.
"TAMWA Zanzibar inawaomba wanawake wa vyama vyengine vyote kujitokeza katika kugombea nafasi mbali mbali ili kuongeza mabadiliko haya ya wanawake katika ngazi za maamuzi itakayopelekea pia kutatuka kwa matatizo mbali mbali yanayowaaathiri kiuchumi na kijamii," amesema.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kujitokeza
wanawake kugombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi kutokana na mifumo dume
ambayo inamtenga mwanamke katika kuwania nafasi za maamuzi sambamba na mwenziwe
mwanamme.
Hadi miaka ya 1940 ilionesha kuwa mwanamke alikatazwa
kuhudhuria hata skuli, nyenzo muhimu katika kukwaa ngazi za kisiasa na kijamii
kwa madai kuwa anaweza kupoteza ujanajike wake.
Hali hii ilirejesha nyuma sana maendeleo ya wanawake na nchi
kwa jumla kwa vile wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi wa Zanzibar kwa
mujibu wa Sensa ya 2012 na makisio ya idadi ya watu yaliyofuata.
Tafiti duniani kote ikiwemo na Zanzibar zinaonesha kuwa
wanawake ni watendaji wazuri, waaminifu, waadilifu na wanaofanya maamuzi kwa
njia ya ushirikishi na hivyo wakiwa kwenye uongozi huharakisha sana maendeleo
ya nchi.
Ni Amina Salim Ali tu ndiye aliyewahi kuomba ridhaa ya
wananchi kupitia chama hicho kikuu nchini mwaka 2000 ambapo hakuweza hata hivyo
kuchaguliwa na hivyo Zanzibar kukosa kabisa mgombea mwanamke pamoja na Rais
mwanamke kwa maisha yote.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464