Na Gaspary Charles - Zanzibar
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) - Zanzibar
kimewapatia mafunzo ya ufugaji wa Kuku Wanawake 10 walioathirika na vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo utelekezaji kisiwani Pemba.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliyojumuisha
waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kutoka Wilaya ya Wete na
Mkoani yamelenga kuwawezesha wanawake kujuendeleza kiuchumi baada ya kukumbana
na udhalilishaji huo.
Mratibu wa Chama hicho Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said
amesema lengo la kutolewa kwa mafunzo hayo ni kuwawezesha Wanawake kujisimamia
kiuchumi baada ya kukumbwa na udhailishaji ikiwemo utelekezaji.
“Tumebaini kwamba sababu kubwa ya kuwepo kwa wimbi la
ubakaji na udhalilishaji katika jamii chanzo chake ni mifarakano ya kifamilia
na utelekezaji, hivyo TAMWA Zanzibar imeamua kuandaa mafunzo haya ili
yawasaidie wahanga wa vitendo hivyo kujishughulisha katika shughuli mbalimbali
za kiuchumi,” Alisema.
Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo, Omar Hamad Mjaka amesema
mafunzo hayo yamekikita kuwapatia mbinu mpya za ufugaji wa kisasa ili uweze
kuwasaidia kuimaisha vipato vyao na kujikimu kiuchumi.
“Mafunzo haya yanalenga kuwapatia elimu na mbinu
mpya za ufugaji wa Kuku kwa kutumia njia bora za kisasa na kuondokana na
ufugaji wa mazoea kwa lengo la kukuza uchumi wa familia.” alisema.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Riziki Said Khatib
ameishukuru TAMWA Zanzibar kwa kuwezesha mafunzo hayo na kwamba yatawasaidia
kujikwamua kiuchumi kutokana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo.
“Tunashukuru sana kwa mafunzo haya, tunaamini kupitia
ufugaji itatuwezesha kujisimamia wenyewe na kuendesha familia zetu ikiwa ni
pamoja na kuwasomesha watoto wetu.” alisema.
Utoaji wa mafunzo hayo kwa Wanawake ni utekelezaji wa mradi
wa Jukwaa la wanahabari la kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar
unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA, Zanzibar kwa
ufadhili wa Danish International Development Agency (DANIDA).
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464