WANAWAKE wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU),
wameiomba Serikali kuingia katika kupambana na ukatili kwa mwanamke hasa
rushwa ya ngono mahali pa kazi.
Hayo yalielezwa jana jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya ushauri
wa wanawake Taifa wa chama hicho, Beatrice Njawa, wakati akisoma risala
katika mkutano wa siku mbili wa viongozi wanawake wa Talgwu kutoka
mikoa yote nchini.
Njawa alisema vitendo vya rushwa ya ngono bado vipo katika baadhi ya
ofisi na imekuwa ni changamoto kwao, hivyo wanaiomba Serikali
kuliangalia jambo hilo kwa umakini.
“Rushwa ya ngono na mfumo kandamizi bado upo kwenye ofisi zetu,
kupitia Talgwu tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili licha ya kwamba
kwa sasa limepungua lakini bado lipo katika baadhi ya sehemu,”alisema.
Alisema changamoto nyingine wanayokutana nayo ni uwakilishi mdogo wa
wanawake katika ngazi ya maamuzi hivyo aliiomba Serikali kuweka mfumo wa
pamoja kuhakikisha wanawake wanakuwa wengi katika ngazi za maamuzi.
Mwenyekiti huyo alisema changamoto zingine wanazokabiliana nazo ni
kusitishwa kwa fao la uzazi, afya na usalama mahali pa kazi huku
akitolea mfano baadhi ya sehemu vyoo kutokuwa rafiki kwa wanawake.
Alisema changamoto nyingine ni mfumo wa kuchagua wategemezi katika
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kutokuwa rafiki kwao kwa kupangiwa watu wa
kupata huduma hiyo.
Kwa upande wa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania,
Pendo Berege alisema changamoto zote wamezipokea na watazifanyia kazi.
Alisema kwamba suala la uwakilishi mdogo kwa wanawake katika ngazi
za maamuzi wamelijadili na wamekubaliana kwamba uwakilishi utaongezwa
na kuonekana.
“Wanawake tunaweza tupeane sapoti kwa sababu kufika tunapopataka ni
sehemu moja ila kuwa msemaji wa mambo yetu ni jambo lingine, bado
tunahitaji kuwa na viongozi wanawake haiwezekani katika vyama vya
wafanyakazi 34 halafu tuna Katibu mmoja tu mwanamke,”alisema.
Naye, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Nchini (Tucta) ambaye pia ni
Makamu Mwenyekiti wa Talgwu, Tumaini Nyamhokya, alisema moja ya jambo
wanalojivunia ni kupambana kuhakikisha darasa la saba wanarudi kazini
pamoja na punguzo la kodi katika mishahara.
“Tulikaa na Waziri wa Fedha na Mipango vikao kadhaa na baadhi ya mambo yameenda vizuri na yameonekana,”alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Talgwu Taifa, Selemani Kikingo, alisema awali
kulikuwa kunachangamoto ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake lakini kwa
sasa umepungua kutokana na matatizo hayo kutatiliwa kuanzia katika
ngazi za chini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464