WALIOKUWA UPINZANI WAKAENDA CCM WALIVYOBWAGWA MAJIMBONI KURA ZA MAONI, DK. MOLLEL ANUSURIKA KWA KURA MOJA


 Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
  Hekaheka za mchakato wa kura za maoni majimboni kuwapata wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu zinazidi kushika kasi, ambapo baadhi ya waliokuwa wabunge kupitia upinzani kisha wakaunga mkono juhudi za serikali na kuhamia CCM kisha kujitosa kwenye mchakato huo wameangukia chali.

Shinyanga Press Club Blog imekuchambulia baadhi ya wanasiasa hao waliojizolea umaarufu kupitia siasa za upinzani lakini baadaye wakajiondoa upinzani na kuhamia CCM lakini kwenye mchakato huu wa kura za maoni wameambulia patumu.

 Joshua Nassari
Katika Jimbo la Arumeru Mashariki nako aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari kisha kuvuliwa ubunge na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameangukia chali baada ya kushindwa kufurukuta kwenye kura za maoni.

Nassari ameshindwa na mrithi wake wa nafasi ya ubunge, Dk. John Pallangyo ambaye ameibuka kidedea katika mchakato huo kwa kura 536, huku Nassari akiambulia kura 26 pekee.
 
David Kafulila 
Katika Jimbo la Kigoma Kusini, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya Chama cha NCCR Mageuzi, David Kafulila na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe ameshindwa kwenye mchakato huo wa kura za maoni.

Kafulila baada ya kutia nia ya kugombea ubunge, uteuzi wake wa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe ulitenguliwa na Rais Dk. John Magufuli.

Kafulila ameshindwa kwenye kura hizo, baada ya mtia nia mwenzake, Hasna Mwilima kuibuka kidedea kwa kupata kura 273, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Nashon Bidyanguze aliyepata kura 143 na David Kafulila akiambulia kura 64.

 Abdallah Mtolea

Katika Jimbo la Temeke mkoani Dar es Salaam, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Mtolea kwa tiketi ya CUF naye katoka chali baada ya kuzidiwa kura na mshindi wa kura hizo, Abbas Mtemvu aliyepata kura 203, huku Mtolea akiambulia kura 22.

Daniel Nsanzugwako

Katika Jimbo la Kasulu Mjini, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako aliibuka kidedea kwa kura 105 akimshinda mwanasiasa mkongwe, Daniel Nsanzugwako aliyeambulia kura 80.
Nsanzugwako alikuwa mbunge wa jimbo.

 David Silinde

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Momba kwa tiketi ya CHADEMA kabla ya kujivua vyeo vyote ndani ya chama hicho kisha kuhamia CCM, David Silinde jana ameangukia patupu katika Jimbo la Tunduma.

Silinde alishindwa kufurukuta mbele ya Aden Mwakyonde aliyeibuka kinara kwa kura 250, wakati Silinde akiibukia katika nafasi ya pili kwa kura 118.
 
Patrobasi Katambi 
Katika jimbo la Shinyanga Mjini, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobasi Katambi amejikuta akishindwa hata kuingia tatu bora baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Stephen Masele kuibuka kinara kwa kura 152.

Katambi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (BAVICHA) kabla ya kuhamia CCM na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya Dodoma lakini alitumbuliwa mapema mwezi Julai, 2020 baada ya kutia nia ya kugombea ubunge.
Dk. Godwin Mollel

Mpaka sasa katika orodha hii, ni Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel ambaye amepenya kwenye kura za maoni baada ya kumshinda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri katika jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.

Dr. Godwin Mollel aliibuka kinara wa mchakato huo akipata kura 148 na kumshinda mshindani wake wa karibu, Aggrey Mwanri aliyepata kura Mwanri 147 akizidiwa kura moja pekee.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464