WAZAZI WAKAMATWA WAKIWAFUNDISHA WATOTO NGONO, MBINU ZA KUISHI NA MME


Baadhi ya wazazi kutoka kata ya Nalasi wilaya ya Tunduru wakipanda Kalandinga (gari) la Polisi baada ya kukamatwa jana wakiwafundisha watoto wao wenye umri chini ya miaka minane masuala ya ngono na kuishi na wanaume vitendo vinavyotajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa ongezeko la mimba za utotoni kwa wasichana wengi katika wilaya hiyo. 

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo,wamefanikiwa kuwakamata wazazi 35 waliokutwa wakiwafundisha watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka 8 mbinu za kuishi na wanaume na kufanya tendo la ngono maarufu kama msondo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro

Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alisema,wazazi hao wamekamatwa nyakati za usiku wakiwa wamejifungia kwenye nyumba mmoja wa waliokamatwa katika Kijiji cha Nalasi wakiwa na watoto hao.

Alisema, wazazi hao wamekamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kwamba,kuna wazazi wamewaficha watoto wa kike wenye umri mdogo na kuwafundisha mila potofu zinazohusiana na mambo ya ngono ambayo hayapaswi kufundishwa watoto wadogo.

Mtatiro alisema,wazazi hao walikamatwa nyakati za usiku wakiwa na watoto hao wadogo wakiwa katika moja ya nyumba iliyokuwa inatumika kwa shughuli hiyo.

Pia alisema,katika msako huo mbali na wazazi hao wamemkamata kungwi mmoja,mtendaji wa Rajabu Lusanga na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nalasi Ali Omari ambao wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wazazi hao licha ya kuishi jirani na eneo la tukio hilo. Wazazi wa kata ya Nalasi wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wakiwa kwenye gari la Polisi baada ya kukamatwa
Kwa mujibu wake shughuli za msondo hazikatwi kufanywa,isipokuwa ni kwa wasichana wakubwa wenye umri zaidi ya miaka 18 na wale wanatarajia kuolewa,badala ya kuwafundisha watoto wadogo ambao hawana uwezo wa kuelewa jambo lolote.

“Natoa wito kwa wazazi wote katika Wilaya ya Tunduru tabia ya kuwafundisha watoto wadogo namna ya kuishi mama na baba jambo hilo tumelipiga marufuku kwani linachangia sana kuongezeka kwa mimba na wasichana wengi kuacha shule”alisema, Mtatiro.

Alisema, vitendo hivyo vinasababisha watoto wadogo wa kike kukosa haki yao ya kupata elimu na kusisitiza kuwa operesheni hiyo itaendelea katika vijiji mbalimbali hadi pale jamii itakapo acha kufanya vitendo hivyo.

Baadhi ya wakazi wa Tunduru wamepongeza jitihada kubwa zinazo fanywa na Serikali ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya kukomesha baadhi ya mira potofu ambazo zimekuwa chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa watoto wa kike wengine kuacha masomo.

Ali Shaibu mkazi wa Nakayaya alisema,jitihada zinazofanywa na DC Mtatiro zinapaswa kuungwa mkono na jamii ya watu wa Tunduru kwani zitasaidia kuepusha mimba za utotoni,kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi na kupoteza vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya familia na Taifa.

Awetu Rashid, ameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua ya kukomesha vitendo hivyo ambavyo kwa muda mrefu vimechangia wilaya hiyo kubaki nyuma kielimu na hivyo kuwa maskini licha ya ukweli kwamba imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464