Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kulia) moja ya zao la kazi za mikono za wanufaika wa huduma zinazotolewa na Hospitali hiyo waliowezeshwa kutengeza bidhaa mbalimbali.
Na Mwandishi wetu
Msajili wa Mashirika Mashirika yasiyo ya
Kiserikali nchini,Vickness Mayao ameeleza kuridhishwa na ubora na viwango vya
huduma zinazotolewa na Hospitali ya CCBRT za kuwahudumia Watanzania
wanaokabiiliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Mayao ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam
alipofanya ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa
shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali sambamba na uhakiki wa matumizi ya
fedha ndani ya mashirika hayo ili kuendana na mwongozo wa mashirika
unayosisitiza uhalisia wa fedha na matumizi yake.
“Hii ni ziara ya kujiridhisha na fedha
zinazotumiwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuhakikisha fedha
zinazoingia kwa jina la Tanzania, zikilenga kuwanufaisha Watanzania zisitumike
kinyume,” alisisitiza
Aliongeza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali
yanatakiwa kuhakikisha fedha zinazotolewa na wafadhili kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali zinatumika kulingana na malengo yake na hivyo kuwanufaisha
walengwa waliokusudiwa.
“Hapa nieleze tu kwamba CCBRT wanafanya kazi
nzuri sana katika huduma zao kwa walengwa na hata katika miradi
wanayoitekeleza, Mfano ni Jengo hili hapa kweli tunaona kwamba wamefanya vizuri
sana,” alisema.
Aidha, amesema kuwa baadhi ya mashirika
yaliyokaguliwa pamoja na kutekeleza majukumu yake, hayatekelezi miradi kwa
ukamilifu wake na hivyo kusababisha maswali na hoja katika matumizi ya fedha
zinazotolewa na wafadhili.
Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya
Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga amesema CCBRT
imekuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma
hasa za afya kwa watu ambao wengi wana kipato cha chini.
“Niseme ukweli, Kazi hii kubwa inayofanywa na
CCBRT ilitakiwa kufanywa na Serikali, Lakini kwa kuwa Serikali imekasimu kazi
hii kwa NGOs kwa utaratibu unaokubalika hivyo ni lazima lazima kazi hizo
kufanyika kwa viwango vikubwa kama inavyofanya CCBRT”alisisitiza.
Pia amefafanua kuwa mwongozo wa Uratibu wa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliotolewa na Serikali hivi karibuni hauna kusudio
la kuyabana Mashirika hayo kama inavyodhaniwa na baadhi wadau bali umelenga
kuweka uwazi katika matumizi ya fedha za miradi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa
CCBRT, Brenda Msangi amesema Hospitali hiyo inafanya kazi kubwa ya
kuwarejesha watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya katika mfumo wa kawaida
ili waweze kufurahia maisha kama walivyo watu wengine.
Brenda amesema kuwa Hospitali ya CCBRT inatoa
huduma mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na upasuaji kwa watu wenye miguu
pinde na kuwapatia vifaa saidizi, upasuaji na urejeshaji wa katika hali ya
kawaida kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na midomo sungura, utoaji wa huduma kwa
wanawake wenye ugonjwa wa fistula pamoja na kutoa huduma nyingine za Matibabu.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kushoto) Msajili wa Mashirika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao (wa tatu kushoto) na Maafisa wengine kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs wakati wa ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WAMJW