AKIMBIZA NGURUWE PORI AKIWA UCHI BAADA YA KUKWAPUA MFUKO WAKE


Wanyama wa mwituni wamekuwa na kawaida ya kujivinjari kwenye maeneo watu wanapokusanyika
Mtu mmoja aliyekuwa hajavaa hata nguo moja alijikuta katika taharuki baada ya nguruwe mwitu kukwapua mfuko wake wa plastiki -ambao ulikuwa na kompyuta mpakato ndani yake.
Mwanaume huyo ambaye alikuwa hana nguo yoyote mwilini mwake alianza kumfukuza nguruwe huyo na vitoto vya nguruwe viwili-jambo lililowaacha hoi kwa kicheko watu wengine ambao walikuwa wakiota jua kama yeye.
Adele Launder, muigizaji, alimpiga picha mwanaume huyo alipokuwa akimfukuza nguruwe mwitu huyo ,katika eneo maarufu, Teufelssee - kisha akaziweka katika mtandao wa Facebook.
''Asili inapokurudi!'' aliandika akiongeza kuwa mwanaume huyu alicheka sana kuona picha zake.
''Alijitahidi kukimbia'', bila nguo yoyote mwilini, alisema bi Launder. ''Kisha nikamuonesha picha, akacheka sana na kuniruhusu kuzichapisha hadharani.''
Kuna utamaduni maarufu wa kukaa watupu nchini Ujerumani kwa baadhi ya watu wanaoamini kuwa kukaa katika hali ya utupu ni jambo zuri kiafya hasa wakati wa majira ya joto, ambapo watu huvua nguo zote kwenye maeneo ya hifadhi, harakati hizo za kurejea katika hali ya asili huitwa kwa kijerumani Freikörperkultur yaani ''utamaduni wa kuupa uhuru mwili''.
Tukio hilo la siku ya Jumatano limetokea siku kadhaa baada ya kuonekana mbwa mwitu mmoja akitembea akiwa na viatu vya watu ambavyo viliachwa bahati mbaya kwenye bustani.
Wakati wa kusalia nyumbani kuepuka maambukizi ya virusi vya corona kulikuwa na ripoti nyingi kuhusu wanyama kuzunguka zunguka katika maeneo ya wazi ya Umma. Nguruwe mwitu wamekuwa wakijivinjari katika baadhi ya maeneo katika viunga vya mji wa Berlin.
Credit BBC Swahili
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464