Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara ya uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Francisca Ngw'endesha akimkabidhi Mwongozo wa uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Rashid Mchata Ofisini kwake.
Na Mwandishi WAMJW-Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WAMJW.
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yametakiwa kuzingatia mabadiliko ya sheria Na.3 ya mwaka 2019 pamoja na mwongozo wa uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuwasilisha Mikataba ya ufadhili na taarifa za utekelezaji kwenye Ofisi ya Msajili wa Mashirika hayo.
Matakwa hayo yametolewa na timu kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Msajili wa NGOs ambayo imetembelea NGOs Mkoani Kigoma kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Mashirika hayo pamoja na uzingatiaji wa sheria na kanuni zake.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs Derek Mwajombe akizungumza kwa nyakati tofauti na uongozi wa mashirika hayo amewasisitiza kuhakikisha kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi, wawasilishe mikataba ya ufadhili kwenye Mamlaka husika, kwa lengo la kuiwezesha Serikali kujua wanafanya nini nchini.
"Lengo ni kuwa Serikali ijue kiasi gani cha fedha, kimeingia, kimetoka wapi na kinakwenda kufanya nini" amesema Mwajombe.
Naye Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Mwandamizi kutoka Idara ya uratibu wa NGOs Musa Leitura amesema kwa mujibu wa Sheria, shirika lolote haliruhusiwi kutekeleza mradi wowote bila kupata idhini ya msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
"Kitu muhimu ni ushirikishwaji na Mwongozo unaeleza namna na kutekeleza vizuri, sheria inatoa wajibu kwa mashirika kuwasilisha mikataba, kwa hiyo huruhusiwi kutekeleza miradi kabla hujapata idhini ya msajili" amesisitza Leitura.
Baadhi ya waratibu wa Mashirika hayo akiwemo Jackob Tunga wa Kigoma Alliance for Community Needs(KACON), ameishukuru timu hiyo kwa kuwaelimisha kuhusu sheria mpya na kuahidi kuitekeleza kwani walikuwa hawafahamu na kuomba Wizara iendelee na utaratibu huo wa kufanya ufuatiliaji.
" Tunashukuru kwa ujio huu kwani umetusaidia kujua umuhimu wa kuwasilisha ada na taarifa, ombi letu, Wizara iendelee kutuma wataalamu kwa ajili ya kutupa elimu" amesema Tunga.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha msaada wa sheria, Kigoma Paralegal Aid Centre (KIPACE) Yasinta Ambrose amesema shirika lao halijapata ufadhili kwa muda mrefu, wanachama wenyewe wanachangiana ili kuwasaidia wananchi ushauri wa kisheria hasa vijijini.
Timu ya ufuatiliaji imetembelea jumla ya Mashirika tisa katika Wilaya ya Kigoma Ujiji.
Timu ya ufuatiliaji wakiwa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma mara baada ya kuwasili Mkoani hapo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Sheria namba 3 ya 2019 ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali
Timu ya ufuatiliaji ikipitia nyaraka mbalimbali za Shirika la KIVIDEA mkoani Kigoma, wakati timu hiyo ikiwa kwenye ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani hapo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464