ASDP II IKISIMAMIWA IPASAVYO TANZANIA ITAZIDI KUPAA KIUCHUMI


Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakikagua mabanda ya maonesho ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo kabla ya uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akionyesha vitabu vya Mwongozo wa Kitaifa wa Uongezaji virutubisho Kibiolojia katika mazao ya chakula wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020. Wengine pichani ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka (Kulia).

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe adam Malima wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Serikali Imesema kuwa endapo Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) itatekelezwa kama ilivyopangwa, Tanzania itakuwa kiuchumi zaidi ya sasa.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 1 Agosti 2020 mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu.

"Tunayo furaha na tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Nchi yetu Mwaka huu kuingia kati ya nchi zenye uchumi wa kati mapema kabla ya lengo lililokuwa limewekwa yaani Mwaka 2025. Jitihada hizo zimechangiwa kwa Sehemu kubwa na wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi yetu kwa kufanya kazi kwa bidii" Amesema

Waziri Hasunga amemuhakikishia Makamu Rais kuwa Wizara za Kisekta zimejipanga kuhakikisha panakuwepo na upatikanaji wa uhakika wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani jambo litakaloimarisha uwezekano wa viwanda vya ndani kuwa na uwezo wa kuchaka Mazao wakati wote.

Kadhalika amesema kuwa Wizara ya Kilimo imeendelea kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.

Ameitaja Mikakati mingine ambayo Wizara inaendelea nayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha mbolea zinapatikana kwa wingi, kwa bei nafuu na kwa wakati, Pamoja na kuhakikisha kuwa inafugwa mifugo kitaalam zaidi ili kupunguza mifugo kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. 

Hasunga amesema kuwa Serikali kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo imedhamiria kuboresha zaidi sekta ya uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa. Aidha, tumejipanga kuhakikisha kuwa kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) sekta ya uvuvi inaongeza ufugaji wa samaki wenye tija na endelevu katika mabwawa ili tuweze kuzalisha samaki wengi zaidi na kuondoa kabisa uvuvi haramu.

"Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele na miongozo ya Kitaifa ili kilimo kichangie kutoa malighafi za viwanda. Amesisitiza

Pia ameyataja maeneo machache, maalum na ya kimkakati katika kilimo ambayo yanafanyiwa maboresho ili kuimarisha usimamizi wa kilimo na kuwapatia Wakulima huduma kwa urahisi zaidi ambayo ni pamoja na usajili wa wakulima, mapitio ya sera ya kilimo kwa lengo la uanzishaji wa Sheria ya Kilimo, uanzishwaji wa bima ya mazao, uimarishaji wa masoko ya mazao ya kilimo, uimarishaji wa mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo sahihi na kwa wakati.

Kauli mbiu katika maonesho ya mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020. Wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii wapo tayari kwa Uchaguzi na kupitia kwako wanatoa salamu zao kuwa kwa mafanikio amabayo serikali ya Awamu ya Tano imepata katika sekta hizi, Ushindi kwa Chama Tawala upo pale pale na utakuwa wa kishindo kikubwa.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Kupitia maadhimisho hayo amesema kuwa Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine wanapata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili hatmae sekta hizi ziweze kuongeza uzalishaji na tija zaidi. Uwekezaji katika sekta ya kilimo ukiwa wenye tija uzalishaji utaongezeka katika eneo dogo na upatikanaji wa malighafi za kutosha utakuwa wa uhakika zaidi. 

MWISHO
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464