ASKOFU MABUSHI, WENZAKE WAIMWAGIA SIFA CCM UTEUZI WA ASKOFU GWAJIMA

Askofu wa kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) Shinyanga, David Mabushi

Na Suzy Luhende, Shinyanga
Askofu wa kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) Shinyanga, David Mabushi  ameupongeza uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kuweka umakini katika kuteua wawakilishi wa chama hicho kwenye nafasi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu ujao, ikiwemo kupitishwa kwa Askofu Josephat Gwajima katika jimbo la Kawe.

Pongezi hizo amezitoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Shinyanga, ambapo amesema uteuzi uliofanyika ni wa haki kwani umezingatia haki kwa kila mmoja hadi kwa viongozi wa dini waliothubutu kugombea.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli pamoja na viongozi wenzake wote wameongozwa na roho mtakatifu katika kutoa maamuzi ya kimungu, hivyo kuchaguliwa Askofu Gwajima na wengine ambao majina yao yamerudi ni mpango wa Mungu.

“Nawapongeza sana CCM kwa namna walivyopata wagombea, safari hii wamejitahidi sana kwa kufanya mchujo hatua kwa hatua nafikiri wamefanya hivyo ili wajipatie watu watakaofaa zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” amesema Askofu Mabushi.

Pia amewaomba wale waliopita kwenye kura za maoni lakini majina yao hayakurudi waweze kuwa na amani watulie kwa sababu kuna namna ambayo imefanyika na kuonekana hawa waliochaguliwa wanafaa kupeperusha bendera ya CCM.

“Nawaombeni wagombea wote walioshindwa kwenye kura za maoni na walioshinda lakini majina yao hayakurudi watulie wawe wavumilivu na waungane na wagombea walioteuliwa katika uchaguzi mkuu, kwani Mungu anajua nini amewaandalia,” amesema Mabushi.

Aidha amesema anaomba kuungana na viongozi mbalimbali wa dini kuiombea tume ya uchaguzi ili iweze kusimamia vizuri uchaguzi uwe wa haki na amani na Mungu atawabariki.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Philadelfia Miracle Tample lililoko Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga,  Leizer Baraka amesema anampongeza Rais kwa kumteua Askofu Josephat Gwajima kwani Mungu amemtumia kwa kuwaona watumishi wa Mungu nao wanafaa kuwepo ndani ya bunge.

Mtumishi wa Mungu kutoka kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Robart Minze amesema viongozi wa chama wamefanya maamzi yao kwa kuongozwa na Roho mtakatifu, hivyo Mungu aendelee kusimama kwa viongozi walioteuliwa kwa sababu ni kwa mapenzi yake.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464