CRDB KANDA YA MAGHARIBI YAKUTANA NA MAWAKALA KUWAJENGEA UWEZO

Mawakala wa benki ya CRDB mkoa wa Geita wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa leo ili kuwajengea uwezo waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Na Shinyanga Press Club Blog
Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi leo Agosti 13, 2020 imekutana na mawakala wake wote kutoka wilaya za Nyang'wale, Geita na Sengerema katika hafla fupi ya kuwajengea uwezo iliyofanyika mkoani Geita na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel.

Mafunzo hayo yalikuwa maalum kuwajengea uwezo mawakala hao kutoka mkoani Geita, ambapo wamepewa mafunzo maalum ya namna ya kufanya kazi zao kwa ufanisi, usalama na kwa kufuata sheria za kibenki. 

Akifungua Semina hiyo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema CRDB ni benki inayofanya vizuri nchini Tanzania, hivyo mawakala waendelee kujituma katika kazi yao ili wajipatie kipato cha uhakika. 

RC Robert Gabriel amewahakikishia mawakala wote wa mkoa wa Geita kuwa hali ya usalama ni shwari hivyo wafanye kazi kwa amani, pia Mhandisi Gabriel amewaahidi mawakala hao kuwa Serikali ya mkoa huo itatenga sehemu maalum kwa ajili ya mawakala wa huduma za kifedha ili waweze kutoa huduma kwenye maonyesho ya Dhahabu ambayo yanatarajiwa kufanyika hivi karibuni mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (katikati) akipokelewa na viongozi wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi kwa ajili ya ufunguzi wa mafunzo hayo


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464