DCI BOAZ AFANYA ZIARA KAHAMA, ATOA MAAGIZO TATIZO LA MIMBA KWA WATOTO


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Kamshina, Robert Boaz (wa pili kulia) akisalimiana na viongozi wa jeshi la polisi wilayani Kahama, wa kwanza Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Kuongezeka kwa Vitendo vya Ubakaji na Ulawiti kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 hususani wanafunzi mkoani Shinyanga umetajwa kuchangiwa jamii kwa kutowafichua watu wanaotekeleza matukio hayo kwa vyombo vya dola pindi yanapotekea na kusababisha wengi wao kukatisha masomo baada ya kupata mimba.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 24, 2020 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Kamshina, Robert Boaz wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani Kahama katika ziara yake ya kikazi ya siku mmoja mkoani Shinyanga ya kukagua utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.

Amesema kuwa bado jamii mkoani humo haitoi ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi ikiwo jeshi la polisi kwa kuwafichua watu wanaotekeleza matukio ya Ubakaji na ulawiti ili hatua za kisheria ziweweze kuchukuliwa kwa wahusika wanaofanya uhalifu huo.

“Ubakaji na ulawiti ni uhalifu, Sisi Jeshi la Polisi tumedhamiria kuutokomeza kwa kushirikiana na wananchi kwani matukio mengi ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 kufanyiwa ukatili huu hujitokeza kwa mara kwa mara ili kuwafichua na waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Boazi

Amefafanua kuwa kwa sasa Jeshi hilo lina idara hiyo maalumu ya Ushirikishwaji wa jamii kwa kila mkoa ambapo kata zote nchini zimepangiwa askari polisi mmoja kwaajili ya kufanya ufauatiliaji wa matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahusika wa uhalifu huo.

“Mimba kwa wanafunzi zimekithiri katika mkoa huu ila wanaotekeleza matukio hayo hatutaki kuwataja ili wachukuliwe sheria,hebu shirikianeni na askari wetu ambao tumewapanga kila kata ambapo kwa sasa wananchi mnaweza kutoa taarifa kuhusiana na matukio hayo kwa njia rahisi katika maeneo yenu mnayoishi,” amesema Kamshina Boaz.

Sambamba na hilo Kamishina Boazi amebainisha kwamba Jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha amani inatawala katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu na viongozi wote wa vyama vya siasa watapewa haki sawa ikiwa ni pamoja na kupewa ulinzi wakati wote wa kampeni,upigaji kura na utangazaji wa matokeo.
DCI Kamishna Robert Boaz akiwasili wilayani Kahama

Gwaride lililoandaliwa kumkaribisha DCI Robert Boaz
 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464