TARIME: HOUSEBOY AFUNGWA KWA KUMLAWITI MTOTO WA MIEZI 17


Mfanyakazi wa nyumbani, Magige Thomas (21), mkazi wa Mtaa wa Rebu Tarime mjini mkoani Mara, amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 5.

Kwa mujibu wa NIPASHE, Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Veronika Mugendi, aliyesikiliza kesi hiyo ya jinai namba 419 ya mwaka 2019.

Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Salum, alidai mahakamani kuwa, mtuhumiwa huyo mnamo Agosti 5 mwaka jana mchana, akiwa mfanyakazi wa nyumbani maeneo ya Bomani, wakati wazazi wa mtoto huyo wakiwa wamekwenda kazini, alimlawiti mtoto wa mwajiri wake na kumsababishia maumivu makali.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanne na kuithibitishia mahakama kuhusiana na kitendo hicho ikiwamo taarifa za polisi (PF3), mganga na wazazi na upande wa utetezi haukuwa na shahidi utetezi uliotolewa na mshtakiwa.

Hakimu Mugendi alisema kuwa, kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama yake, anaungana na upande wa mashtaka na kumtia hatiani mtuhumiwa Magige na kumhukumu kwenda kutumikia kifungo cha maisha jela, ili liwe fundisho kwa watu wenye nia ovu na wasio na huruma na watoto.

Licha ya mshtakiwa kuiomba mahakama kumsamehe makosa yake au kumpa adhabu ndogo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi Salum aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa kuwa kitendo alichokifanya ni cha kinyama.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mtuhumiwa alionekana akitokwa machozi, huku wananchi waliokuwa wamefurika mahakamani hapo kufuatilia hukumu hiyo, wakisikika wakisema ‘haki imetendeka’.

Kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya watoto nchini, baadhi ya wataalamu wa saikolojia na ustawi wa jamii wakidai hali hiyo inachagizwa na mambo mengi zikiwamo imani za kishirikina na jamii kutokuwa na hofu ya Mungu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464