Kikosi maarufu cha timu ya taifa ya Cameroon ambacho kilifika hatua ya robo -fainali kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka 1990 nchini Italia , hatimaye watapata nyumba zao walizoahidiwa na Rais Paul Biya miaka 30 iliyopita.
Hatua hii inafikiwa wakati wachezaji watatu , Louis Paul Mfede, Benjamin Massing na Stephen Tataw wakiwa wameaga dunia.
Zoezi hilo limechukua muda mrefu kwa kuwa majina 44 yalikusanywa, badala ya wachezaji 22 wa kikosi hicho.
Ombi kwa ajili ya wachezaji 22 pekee liliwasilishwa, lakini waziri wa wakati huo alibadilishwa kisha suala lenyewe hatimaye likasahaulika.
Chama cha wachezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon, kinachoongozwa na Bertin Ebwelle, kiliibua tena suala hilo katika barua iliyoandikwa kwenda kwa rais wa nchi hiyo mwezi Juni.
Siku ya Jumatano Rais Biya alitia saini waraka kuelekea kwa Mkurugenzi wa shirika la nyumba kuhusu ruhusa kwa wachezaji hao wa zamani kupatiwa nyumba zao
Nyumba hizo ziko katika mji mkuu wa nchi hiyo, Yaoundé, mji wa kibiashara Douala na mji pwani wa nchi hiyo, Limbe.
Roger Milla, mchezaji wa zamani mashuhuri nchini Cameroon ambaye pia ni mchezaji mkubwa kuliko wote katika kikosi hicho cha zamani amemshukuru Kiongozi wa nchi hiyo kwa'' heshima ya kuwatambua''.