MAANDALIZI SHINYANGA SUPER QUEENS YAZIDI KUNOGA, JAMBO PRODUCTS YAJITOSA

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Jambo Food Products, Amina Rashid (kushoto) akimkabidhi jezi Nahodha wa timu ya Shinyanga Super Queens, Tatu Abbas 

Na Shinyanga Press Club Blog
Maandalizi ya timu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Shinyanga Super Queens kwa ajili ya michuano ya Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara kwa soka la wanawake yamezidi kupamba moto, baada ya Kampuni ya Vinywaji ya Jambo Products ya mkoani Shinyanga kuongeza nguvu katika maandalizi hayo kwa kusaidia vifaa mbalimbali ikiwemo jezi za kisasa.

Shinyanga Super Queens ambayo ni timu pekee ya soka mkoani Shinyanga, inajiandaa na ligi daraja la kwanza ili kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL) msimu ujao.

Timu hiyo imekabidhiwa vifaa hivyo leo Agosti 10, 2020 katika ofisi kuu za kiwanda hicho Ibadakuli, mjini Shinyanga, ambapo akizungumzia maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Shinyanga Super Queens, Flora Gaguti amesema timu iko vizuri na imara kushiriki vyema ligi hiyo na matarajio yake ni kuupaisha mkoa huo katika medani za soka la wanawake kwa ushindi na kupanda daraja kwenda ligi kuu. 
Mkurugenzi wa Shinyanga Super Queens, Flora Gaguti (aliyeshika mic) akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada wa jezi

Shinyanga Super Queens ilikabidhiwa vifaa hivyo na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Jambo Food Products, Amina Omary Rashid, ambapo amesema lengo la msaada huo ni  kuwapa hamasa wachezaji kufanya vizuri katika ligi hiyo.

"Msaada huu hautoshi, tunapenda kuona wadau wengine wakijitokeza kuisaidia timu hii ambayo imeonyesha nia ya kung’arisha nyota ya mkoa wa Shinyanga katika medani za mpira wa soka la wanawake," amesema Amina. 

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Shinyanga Super Queens, Henry Moroto ametamba kuwa timu yake iko imara na hakuna timu itakayoizuia kuubeba ushindi wa ligi hiyo, huku wachezaji nao wakitamba kuchukua ubingwa wa ligi hiyo inayotarajiwa kuanza siku za karibuni. 
Mwakilishi wa kampuni ya Jambo Food Products, Amina Rashid akizungumza baada ya kampuni hiyo kuikabidhi msaada wa jezi timu ya wanawake ya Shinyanga Super Queens
Kocha Mkuu wa Shinyanga Super Queens, Henry Moroto
 Nahodha wa Shinyanga Super Queens, Tatu Abbas akishukuru baada ya timu yake kupata msaada wa jezi
 Wachezaji, viongozi wa Shinyanga Super Queens na wawakilishi kutoka Kampuni ya Jambo Food Products wakiwa katika picha ya pamoja baada ya makabidhiano hayo
Wachezaji wa Shin yanga Super Queens


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464