MAHAKAMA KUSIKILIZA UTETEZI WA HALIMA MDEE SEPTEMBA 7

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la CHADEMA, Halima Mdee

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Septemba 7, 2020 itasikiliza utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo Agosti 12, 2020 lakini ilishindikana kwa kuwa mawakili wa utetezi hawakufika mahakamani. 

Mdee alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa mawakili wake, Peter Kibatala na Hekima Mwasipu hawakuwepo mahakamani hapo kwa sababu walikuwa kwenye kesi nyingine Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara na Kazi.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya mshitakiwa kuanza kujitetea. Simon alidai kuwa kwa kuwa mawakili wa mshitakiwa huyo hawakuwepo mahakamani hapo aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya utetezi.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, 2020 kwa utetezi, Mdee anadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya CHADEMA mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, alitenda kosa la kutoa lugha chafu.

Inadaiwa kuwa Halima alitamka maneno machafu dhidi ya Rais John Magufuli na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464