MAKAMU WA RAIS AZITAKA WIZARA NA TAASISI KUKUTANA NA WADAU KUTATUA CHANGAMOTO



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akionesha moja ya miongozo ya Kilimo aliyoizindua katika uzinduzi wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika kitaifa Mkoani Simiyu.

Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara na Taasisi za Umma na binafsi kuwa mstari wa mbele kutafuta na kuwakutanisha wadau wa sekta husika kujadili changamoto katika sekta husika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema hayo leo Mkoani Simiyu wakati akizindua maonesho ya Kilimo, Mifugo na uvuvi Nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi.

Ametaja baadhi ya changamoto zilizopo kuwa ni pamoja na miundombinu ya usafirishaji, upatikanaji wa mitaji, maeneo ya uwekezaji.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza majadiliano ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto yafanyike katika viwanja vyote vya maonyesho nchini ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu na kunufaika na elimu inayotolewa.

Aidha, Makamu wa Rais, ameviagiza Vitengo na Idara za Mawasiliano Serikalini kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu na manufaa ya maoñyesho yanayoendelea kote nchini.

Katika hatua nyjngine, Makamu wa Rais amewakumbusha Wananchi kushiriki katika uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

“Nayasema haya kwa kuzingatia kuwa maonesho ya Kilimo Nane Nane mwaka huu kauli mbiu yake inalenga kuwakumbusha Wakulima, wafugaji na wavuvi kote nchini kuchagua viongozi Bora,” alisema

Hata hivyo, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kufanya Kampeni kwa kuzingatia taratibu zinazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi vinginevyo, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wakakaofanya kampeni zinazolenga kujenga chuki na kuvuruga amani iliyopo.

Akizungumzia maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu, Makamu wa Rais ameeleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wizara za kisekta kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za utafiti, mabenki na sekta binafsi.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua moja ya mabanda katika maonesho ya Nane Nane yanayoendelea Mkoani Simiyu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka wakifuatili Burudani kutoka Kwaya ya AIC wakati wa Uzinduzi wà Maonesho ya Nane Nane.

  Baadhi ya Wananchi walioshiriki Uzinduzi wa Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane uliofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu yaliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya washiriki wa maonesho ya Nane nane Mkoani Simiyu wakimsikiliza Afisa Sheria Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Faki Shaweji akiwaelimisha kuhusu usajili na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.

Afisa Ustawi Mkuu kutoka Wizara ya Afya, ÃŒdara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Amina Mafita akiwasikiliza Wananchi waliofika kwenye banda la Wizara latika maonesho ya Nane nane Mkoani Simiyu. Mwenye Kofia ni Afisa Maendeleo Mkuu, Erasto Ching'oro.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464