Mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobasi Katambi (kushoto) akikabidhiwa fomu na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Geoffrey Mwangulumbi (kulia) leo Agosti 22, 2020.
Na Damian Masyenene– Shinyanga Press Club Blog
HATIMAYE leo Jumamosi Agosti 22, 2020 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobasi Katambi amefika ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo kuchukua fomu, huku akisindikizwa na wanachama wa chama hicho.
Katambi alifika katika ofisi hizo katika Manispaa ya Shinyanga saa 5:10 asubuhi na kukabidhiwa fomu hiyo na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geofrey Mwangulumbi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kisha kuzungumza katika mitaa mbalimbali ya mji wa Shinyanga na baadae kuelekea ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini kuzungumza na kuwashukuru wanachama.
Akimkabidhi fomu, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geofrey Mwangulumbi amemtaka kuhakikisha anarejesha fomu hiyo ndani ya wakati (kabla ya saa 10:00 jioni).
Mwangulumbi pia ametoa angalizo kwa wanasiasa kwa kuwataka watangulize sera za uhakika na nzuri kwa kuweka mbele amani ya nchi, huku wakitakiwa kudhibiti vurugu kwenye kampeni zao.
Akizungumza na wanachama wa CCM katika ofisi za chama hicho wilaya ya Shinyanga Mjini, Katambi amesema kazi yake kubwa ni kuyapigania maendeleo ya wananchi na kuwaunganisha, huku akikishukuru chama hicho kwa kumuamini na kumpitisha kuwa mgombea.
“Sasa ni kipindi cha sisi kuungana na kuwa wamoja tupigane na matatizo yanayotukabili ikiwemo magonjwa na uchumi, nimekuja kuwa mtumishi na siyo ‘Boss’, nawaahidi utumishi uliotukuka, tutahakikisha kwa kipindi chote nitayapigania maslahi ya wana Shinyanga.
“Nitapita kila kijiwe na kila kituo kuchukua hoja na maoni yenu ya changamoto mbalimbali, niliutosa ukuu wa wilaya kwa ajili yenu kwa sababu nilishindwa kuvumilia kuona wananchi wangu wa Shinyanga wanateseka,” amesema.
Katambi amesema atatumia nguvu, akili na mbinu zake zote kwa kushirikiana na chama chake kuwaletea maendeleo wana Shinyanga, na kwamba atakuwa mkali pale atakapoona wananchi wanaonewa,
Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Agness Bashemu aliwashukuru wanachama kwa namna walivyomuunga mkono Katambi, ambapo aamewaomba kuendelea kumpa ushirikiano wakati wa kampeni, huku Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Abubakar Gulam amesema watahakikisha kwamba maamuzi yaliyofanywa juu ya Katambi ni sahihi na atashinda ubunge wa jimbo hilo kwa kishindo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geoffrey Mwangulumbi (kulia) akimkabidhi fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo, Mgombea wa CCM, Patrobasi Katambi (kushoto)
Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Shinyanga Mjini, Geoffrey Mwangulumbi (kulia) akitoa maelekezo kwa mgombea wa CCM, Patrobasi Katambi wakati wa zoezi la kumkabidhi fomu
Patrobasi Katambi (kulia) pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam wakitoka katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini leo
Patrobasi Katambi (kulia) akizungumza na baadhi ya wana CCM waliojitokeza kumuunga mkono wakati wa kuchukua fomu
Patrobasi Katambi akiwapungia mkono wananchi katika mitaa ya Manispaa ya Shinyanga wakati akitoka kuchukua fomu ya kugombea ubunge
Katambi akisalimiana na baadhi ya wananchi wakati wa msafara wake uliokuwa ukitoka kumsindikiza kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Agness Bashemu akizungumza na wana CCM wakati wa kumpokea mgombea ubunge wa chama hicho, Patrobasi Katambi