Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando.
NA: EATV
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekanusha taarifa za kumkamata kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Tunduma Boniface Mwakabanje, kama ilivyoandikwa mitandaoni na kwamba kama kuna mtu ana namba zake basi ampigie ili kujua kama yuko ndani.
Akizungumza na EATV&EA Radio Digital leo Agosti 24, 2020, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando, amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote kwa kuwa Mwenyekiti huyo hajakamwatwa na kwamba hata kama Jeshi la Polisi linafanya utaratibu wa kumkamata lakini bado hajakamatwa.
''Mbona hajakamatwa, mimi ninavyofahamu hajakamatwa kama una simu yake mpigie umuulize akwambie yuko ndani, mimi ndiye RPC wa songwe ninavyokwambia sasa hivi Mwenyekiti wa CHADEMA Tunduma hajakamatwa'', amesema RPC kyando.
Kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter, Mgombea Urais wa CHADEMA Tundu Lissu aliandika kuwa, ''Jeshi la Polisi Tunduma Mkoa wa Songwe limemkamata Mwenyekiti wa CHADEMA Tunduma na mgombea Udiwani Kata ya Majengo Boniface Mwakabanje, na linawatafuta wagombea wengine wanne kwa tuhuma za uongo za uraia, licha ya njama hizi, CCM Songwe haitakwepa kimbunga cha Uchaguzi Mkuu huu''.