Kikosi cha Shinyanga Super Queens
Na Shinyanga Press Club Blog
Nyota Njema imeanza kuonekana kwa wawakilishi wa soka la wanawake Mkoa wa Shinyanga, Timu ya Shinyanga Super Queens inayoshiriki michuano ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwa soka la Wanawake (WFDL), baada ya leo kuianza vyema michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 3 kwa 1 dhidi ya Mkwawa Queens ya Iringa.
Michuano hiyo ambayo ndiyo hupandisha timu mbili zitakazocheza Ligi Kuu msimu ujao, inashirikisha timu 21 kutoka mikoa mbalimbali ambazo zimegawanywa katika makundi manne, ambapo Shinyanga Super Queens iko kundi C lenye timu za Viva Queens, Mkwawa Queens na MT Hanang.
Ligi hiyo imeanza leo Jumatatu jijini Dodoma ambapo inafanyika katika viwanja vya Puma Shelly na Fountain Gate.
Katika mchezo huo, Shinyanga Super Queens wanaonolewa na Kocha Henry Moroto walianza kwa kutanguliwa baada ya kufungwa bao la mapema, hata hivyo vijana hao ambao wamecheza michezo kadhaa ya kirafiki na kufanya maandalizi mazuri, waliinuka na kusakata kabumbu safi ambalo liliwapa mabao matatu ya ushindi yakifungwa na Irine Chitanda, Veronica Mbizo na la tatu wakijifunga Mkwawa Queens.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464