SIMBA SC YATWAA UBINGWA KOMBE LA SHIRIKISHO IKIICHAPA NAMUNGO 2-1


Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog
WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC, leo Agosti 2, 2020 wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) maarufu kama Kombe la FA baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo wa fainali uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoa wa Rukwa.

Simba walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Luis Miquissone 'Konde Boy' mnamo dakika ya 27 kabla ya Nahodha John Bocco kufunga la pili mnamo dakika ya 39 na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0, huku Namungo wakirudi kipindi cha pili kwa nguvu kujaribu kusawazisha mabao hayo, ambapo walifanikiwa kupata goli la kufutia machozi lililofungwa na Edward Charles na kufanya mchezo huo umalizike kwa Simba kushinda mabao 2-1.

Mbali na kukabidhiwa kombe hilo, Wekundu wa Msimbazi pia walikabidhiwa hundi ya Sh Milioni 50 kama zawadi ya mshindi wa michuano hiyo ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo na kupewa kitita cha Sh 500,000 kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo, huku Mzambia Clotus Chama akiibuka mchezaji bora wa mashindano hayo.

Pia Mshambuliaji wa timu ya Panama FC, Omary Yassin ameibuka mfungaji bora wa michuano hiyo kwa akiweka kambani mabao 9

Ubingwa huo walioupata Simba leo unakamilisha safari yao ya msimu wa mwaka 2019/2020 wakiweka kibindoni mataji matatu ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, huku Namungo FC ukiwa na mchezo wao wa kwanza wa fainali kwenye michuano hiyo ikiwa ni mara yao ya kwanza kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakimaliza pia katika nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la shirikisho barani Afrika.
Wachezaji wa Simba SC wakishangilia ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam
 Wachezaji wa Simba SC wakishangilia moja ya mabao waliyoyafunga kwenye mchezo huo
 Kiungo wa Simba SC, Clotous Chama akipokea tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya kombe la Shirikisho kutoka kwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson
 Muonekano wa kombe hilo
Mchezaji wa Simba SC, Luis Miquissone (kushoto) akikabidhiwa zawadi ya mchezaji bora wa mchezo huo wa fainali
Picha kwa hisani ya Simba SC Tanzania
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464