CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza orodha mpya ya wagombea ubunge wake, huku jijini Dar es Salaam kukitawaliwa na safu ya kinamama.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, Tumaini Makene, katika orodha hiyo mpya ya wagombea ubunge 37 wa Tanzania Bara aliyoitoa jana, wamo kinamama 11. Kati yao, wamo watatu wanaofanya idadi ya wagombea wanawake Dar es Salaam kufikia watano.
Kwa mujibu wa Makene, chama hicho hakijateua wagombea katika majimbo Kibamba, Temeke na Ilala jijini kutokana na sababu mbalimbali.
Makene alibainisha kuwa, Temeke na Ilala ni miongoni mwa majimbo saba ambayo chama hicho kitalazimika kurudia mchakato wa kura za maoni wakati Kibamba ni miongoni mwa majimbo saba ambayo CHADEMA haijapiga kura za maoni kuwapata wagombea wake.
Makada wanaume waliochomoza katika uteuzi huo wa CHADEMA jijini Dar es Salaam ni aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, anayewania ubunge wa Ubungo na John Mrema, anayesaka ubunge wa Segerea.
Vilevile, taarifa za chama hicho zinaonyesha kuwapo kwa wateule wengi wanawake wanaopeperusha bendera ya CHADEMA katika majimbo ya miji mikubwa, ikiwamo Shinyanga Mjini, Mpanda Mjini, Morogoro Mjini, Tarime Mjini, Geita Mjini, Bunda Mjini na Tabora Mjini.
Orodha ya kwanza iliyotolewa Jumapili na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila, ilionyesha mageuzi ya kinamama kuchomoza wakiwa jumla ya wateule 40 kati ya 163.
Katika orodha iliyotolewa jana, wanawake waliochomoza katika majimbo ya Dar es Salaam ni Susan Lyimo (Kinondoni), Khadija Mwago (Mbagala) na Lucy Magereli (Kigamboni).
Makada wanawake wa CHADEMA waliokuwamo kwenye orodha ya kwanza ya wateule wa chama hicho kuwania ubunge majimbo ya Dar es Salaam ni Asia Msangi (Ukonga) na Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho (BAWACHA), Halima Mdee anayewania tena ubunge wa Kawe.
SIRI KINAMAMA KUTAMBA
Alipoulizwa na Nipashe jana kuhusu siri ya wanawake kung'ara katika uteuzi wa wagombea ubunge mwaka huu kupitia chama hicho, Makene alianika sababu mbili.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, sababu ya kwanza ni mkakati wa muda mrefu wa chama hicho kuandaa viongozi, ambao alidai umekumbwa na misukosuko mingi ikiwamo kufuatiliwa na vyombo vya dola.
Makene aliitaja sababu ya pili kuwa ni programu mahsusi ya BAWACHA kuhamisha wanawake kujitosa katika uongozi, akifafanua kwamba, "siyo jambo la kubahatisha, liliandaliwa kwa muda mrefu na viongozi wa BAWACHA wamekumbana na mengi, ikiwamo kupigwa mabomu.
Taarifa ya jana ya Makene ilibainisha kuwa Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliyeshika nafasi ya pili katika kura za maoni kumsaka mgombea urais kupitia chama hicho, atagombea ubunge wa Singida Kaskazini.
Mbali na kinamama waliong'ara katika uteuzi wa majimbo ya Dar es Salaam, orodha ya jana ya CHADEMA ilikuwa na majina ya Jacqueline Swai (Ngorongoro), Khadija Madwanga (Kwimba), Neema Chozaile (Geita Vijijini), Salome Makamba (Shinyanga Mjini), Jedidia Kitundu (Msalala), Aisha Madoga (Dodoma Mjini), Hadija Maula (Mvumi) na Cecillian Ndossi (Monduli).
Wengine ni Joel Hema (Singida Mashariki), Martin Mussa (Tabora Kaskazini), Gibson Ole-Meiseyeki (Arumeru Magharibi), Gervas Sulle (Mbulu Mjini), Aboubakar Mashambo (Bumbuli) na Norbeet Marandu (Handeni Mjini).
Vilevile, Nicholous Mapunda (Peramiho), Renatus Nzemo (Bukombe), Gody Bagamba (Mbogwe), Adolf Mkono (Karagwe), Thedo Assechekamwati (Kahama), Emmanuel Magema (Ushetu), Idd Amri (Kishapu), Edson D’zombe (Lupembe), Frederick Kihwelo (Mafinga Mjini), Emmanuel Lusambo (Mpanda Vijijini), James Lembileki (Ludewa) na Peter Mdidi (Mvomero).
Pia wamo Issa Chilindima (Newala Mjini), Arfat Kadewele (Tunduru Kusini), Marato Marwa (Butiama), Larazo Maige (Uliyankulu), Philbert Macheyeki (Urambo) na Nyenje Undi (Tunduru Kaskazini).
Orodha hiyo ya jana ilifanya jumla ya wagombea walioteuliwa na CHADEMA kuwania ubunge kufikia 200. Tanzania ina majimbo ya uchaguzi 264. Kati yake, 214 yako Tanzania Bara na 50 yako Zanzibar 50.
CHANZO -ippmedia.comKama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464