Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya inamchunguza Adam Hussein Simbaya wakala wa mgombea wa nafasi ya viti maalum UVCCM mkoa wa Mbeya kupitia wilaya ya Chunya, Sarah Joel Sompo kwa kosa la kushawishi baadhi ya wajumbe wa baraza za UVCCM mkoani humo kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Julai 31, 2020 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi, wakala huyo alikamatwa Julai 30, 2020 katika ukumbi mdogo wa Mkapa akiwashawishi baadhi ya wajumbe ambao ni wapiga kura ili wampigie kura Bi Sarah kwa miadi ya kuwapatia fedha baada ya zoezi la uchaguzi kukamilika.
Baada ya kumpekuwa alikutwa na fedha kiasi cha Shilingi 810,000 pamoja na note book mbili zenye baadhi ya majina ya wajumbe, ambapo taarifa kamili itatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.
Matechi amewashukuru wananchi wa mkoa wa Mbeya kwa kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.
"Tunawaomba waendelee kuwasilisha taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwa kupiga simu namba 113, kuandika ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au kubonyeza *113# na kufuata maelekezo Huduma hizi zinapatikana BURE kwa mitandao yote ya simu," alisema.