USIKU WA TUZO ZA VPL: SIMBA YABEBA TUZO TANO, YANGA YAAMBULIA SH MILIONI 45



Viongozi wa Simba wakikabidhiwa hundi ya Sh Milioni 100 kama zawadi kwa mshindi wa kwanza (bingwa) wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara

Na Damian Masyenene, Shinyanga Press Club Blog 
MABINGWA wa soka nchini Tanzania, Klabu ya Simba SC ya Jijini Dar es Salaam imeumaliza msimu kwa kishindo baada ya kufanikiwa kushinda tuzo 5 kwenye usiku wa tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom(VPL) Tanzania Bara zilizotolewa Agosti 7, 2020 ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Tuzo hizo zinakuwa sehemu ya mafanikio ya Simba SC msimu huu wa 2019/2020 baada ya kuumaliza wakiwa wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Tuzo ya Kwanza kwa klabu ya Simba ni ya mfungaji bora wa Ligi Kuu na kiasi cha hundi ya Fedha (Sh 10,000,000) imechukuliwa na Meddy Kagere na kupokelewa na Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu. 

Simba pia imekabidhiwa zawadi ya Sh Milioni 100 kama 
mshindi wa kwanza wa Ligi Kuu Vodacom.

KOCHA BORA: Tuzo ya kocha bora imekwenda kwa Sven Vandenbroeck wa Simba akiwashinda Hitimana Thierry wa Namungo FC na Aristica Cioaba wa Azam FC na. 

GOLIKIPA BORA: Tuzo ya golikipa bora imekwenda kwa Aishi Manula wa Simba akiwashinda Daniel Mgore wa Biashara United na Nouridine Balora wa namungo FC. 

KIUNGO BORA: Tuzo ya kiungo bora imekwenda kwa Clatous Chama wa Simba SC akiwashinda Lucas Kikoti wa Namungo FC na Mapinduzi Balama wa Yanga. 

Clatous Chama kutoka Simba SC amechukua tuzo ya mchezaji bora wa msimu akiwashinda Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union na Nico Wadada wa Azam FC. 

Licha ya kuingiza wachezaji watano kwenye tuzo hizo, Klabu ya Yanga haikufua dafu kwani hakuna mchezaji wake aliyefanikiwa kubeba tuzo, bali timu hiyo imeambulia zawadi ya mshindi wa pili ambayo ni hundi ya Sh Milioni 45.


 Viongozi wa Yanga wakikabidhiwa hundi ya Sh Milioni 45 kama zawadi ya mshindi wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara

Picha kwa hisani ya Clouds Digital


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464