Wapelelezi wamepata visanduku vyeusi vya ndege iliyoanguka katika uwanja wa ndege jimbo la Kusini mwa India Kerala na kusababisha vifo vya watu 18.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737 iliyokuwa ikitoka Dubai, ilianguka wakati ikitua katika uwanja wa ndege wakati huo mvua ilipokuwa ikinyesha , kisha kuvunjika vipande viwili, katika uwanja wa ndege wa Calicut maafisa wa safari za anga wameeleza.
Ndege hiyo ilikuwa ikiwarudisha nyumbani raia wa India ambao walishindwa kurejea kutokana na janga la virusi vya corona.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema ''ameumizwa na tukio hilo''.
Shughuli za uokoaji sasa zimekamilika , na anusura wamepelekwa hospitali Calicut na Malappuram kwa mujibu wa Kiongozi wa jimmmbo hilo Pinarayi Vijayan.
Watu kadhaa wamejeruhiwa, 156 kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya, maafisa wameeleza.
Shirika la India Express limesema marubani wawili ni miongoni mwa waliopoteza maisha.
Waziri wa masuala ya anga Hardeep Singh Puri alitembelea eneo la ajali Jumamosi, ambapo alitangaza kupatikana kwa vinasa sauti vya chumba cha marubani na cha kurekodi data, ambavyo ni muhimu katika uchunguzi wa tukio hilo.
''Tunapaswa kuwa na shukrani kwa kuwa madhara si makubwa sana,'' alisema.
''Ndege ilianguka umbali wa futi 34 (mita 10) chini na watu waliweza kufika haraka na kuwatoa watu waliokuwa wamenasa ndani.''
Afisa mmoja ambaye hakutajwa jina aliiambia AFP; ''Mafuta yalivuja ,ulikuwa muujiza kuwa ndege haikushika moto, idadi ya waliopoteza maisha ingekuwa kubwa zaidi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464