Msaidizi wa Sheria Wilaya ya Mkoani- MDIPAU, Shaaban Juma Kassim akiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa vitendo vya vya udhalilishaji wakati wa kikao hicho.
Na Gaspary Charles- TAMWA Zanzibar
MTANDAO wa kupinga udhalilishaji Wilaya ya Mkoani Pemba umefanikiwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuripoti kesi za udhalilishaji na kutoa ushahidi mahakamani kwa zaidi ya wanajamii 2,060 katika Shehia 22 za Wilaya hiyo kuanzia mwezi Mei hadi Augusti mwaka huu.
Wajumbe wa mtandao huo wamebainisha hayo wakati wa kikao cha uwasilishaji ripoti ya ufuatiliaji wa vitendo vya vya udhalilishaji katika ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA ZNZ Pemba.
Walisema katika kipindi hicho wajumbe wa kamati hizo waliandaa mikutano ya utoaji wa elimu katika makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo Skuli, Misikitini kwenye shehia pamoja na urushaji wa vipindi kupitia redio za kijamii.
Aidha walibainisha kuwa kupitia utoaji wa elimu katika jamii juu ya athari za vitendo vya udhalilishaji na ushajihishaji wa jamii kuripoti kesi hizo zinapotokea, hatua hiyo imeanza kuleta mabadiliko katika jamii.
Shaaban Juma Kassim Kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Mkoani MDIPAU alisema kutokana na juhudi hizo za kutoa elimu kwa wanafunzi wameanza kuelewa athari za udhalilishaji na namna ya kuripoti
kesi hizo.
“Baada ya kuchukua juhudi hizi za kwenda kutoa elimu mashuleni, tunashukuru hivi sasa wanafunzi wameanza kuelewa udhalilishaji na matukio yamepungua kwa baadhi ya shehia,” alisema.
Kwa upande wake Abdalla Saleh Issa kutoka jumuiya ya maendeleo ya vijana -YACDES amesema kupitia utoaji wa elimu ya stadi za maisha kwenye jamii wamefanikiwa kuwaunganisha zaidi ya vijana 15 kujishughulisha katika
shughuli za ujasiriamali.
“Tuliandaa utaratibu wa kutoa elimu ya stadi za maisha kwenye jamii na kufanikiwa kuwafikia vijana 15” alisema.
Mratibu wa Chama cha Waadishi wa Habari wanawake TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamtandao huo kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.
“Niwaombeni tuendelee na juhudi hizi za kuielimisha jamii na kuwasaidia wahanga wa vitendo hivyo kupata haki zao bila kuogopa vikwazo vinavyotukabili kwani jamii inahitaji msaada wetu,” alisema.
Kikao hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuongeza nguvu kwenye juhudi za mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa ufadhili wa Finland.