WANAOISHI NYUMBA ZA NYASI WACHANGISHANA NA KUJENGA ZA BATI

Kina mama wa kikundi cha kusaidiana wa Kijiji cha Mondo wilayani Misungwi  Mkoani Mwanza wameondokana na umasikini na kuacha kuishi nyumba za nyasi baada ya kuunda vikundi vya kuchangiana ujenzi wa nyumba za kudumu za bati.

Getruda Luchangula mmoja wa wanufaika wa vikundi hivyo amesema awali walikuwa wakiishi maisha ya umasikini huku chumba kimoja wakilala familia nzima na kueplekea kipindi cha masika kusumbuliwa na wadudu kama mbu na kunguni.

Amesema mabadiliko hayo yameanza mwaka 2016 walipoanzisha kikundi kiitwacho witogwa ( tunapendana) ambapo hadi sasa wameshawajengea watu 12 nyumba za kudumu na kuachana na kuishi katika nyumba za nyasi.

"Kikundi chetu tunachangiana elfu 12 kwa mwezi tupo watu 18, kila mwaka tunawajengea watu wawili nia yetu ni kuondokana na nyumba za nyasi na kuweka nyasi hakika tumefanikiwa na maisha yetu ni bora kwa sasa" amesema na Reuben Lomuu mmoja wa wanufaika wa mpango huo.

  Akizungumza na wananchi hao Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu amesema nyumba bora zinaleta maisha bora hivyo wananchi hao wamefanya kazi kubwa kwani walikuwa kwenye makazi duni ,nyumba duni lakini kwa sasa wanaishi kwenye nyumba nzuri na za kudumu.

 Dkt. Jingu ameongeza kuwa pia utaratbu walioweka wa kuvuna maji ya mvua kwa kila nyumba wanazojenga  ni nzuri na wenye tija kupitia vikundi hivyo watapata urahisi wa kupata mikopo ambapo fedha hizo zikitumika vizuri zinaweza kuleta mapinduzi katika maisha.

" Wote mnaunga kauli ya Rais Magufuli ya tukiamua tunaweza hivyo wakati huu ni wakuchapa kazi ili kuleta maendeleo na tutaendelea kuwaunga mkono ili kuwawezesha na kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali " amesema Dkt. Jingu

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amevishukuru vikundi hivyo kwa kufanya kazi nzuri  na kubwa na kwamba hiyo ni dalili ya kuonyesha Misungwi imedhamiria kuondoa nyumba za nyasi na kuweka bati hivyo alitoa wito kwa wananchi wengine kutumia vikundi vya akina mama kujiletea mafanikio.

  Nestory Mayala ni Mwenyekiti wa Kijiji hicho amesema kwa sasa wananchi wanapenda mabadiliko baada ya kupatiwa elimu ambapo kaya 400 zilizopo kaya 150 zimeweza kujenga nyumba bora.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali Kivulini, Yassin Ally amesema jambo la maendeleo linahitaji uhamasishaji ili kuleta hamasa na stadi za uamusho kwa wananchi hao huku wakina mama wakiwa ndio njia ya kufikia mafanikio hayo sambamba na kupinga ukatili.

"Sisi tunakaulimbiu ya nyasi ni ya kula ng'ombe sio ya kulala binadamu tunatupa nyasi tunaweka majani Lengo ni kujenga na  kuboresha maisha ya kila mwananchi na kuondokana na umaskini" amesema Ally.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464