Aliyekuwa Beki wa klabu ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto (kushoto) akisaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Yanga leo Agosti, 2020.
Na Damian Masyenene, Shinyanga Press Club Blog
IKIWA ni siku moja tu tangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufungua dirisha la usajili Agosti 1 hadi 31, 2020, tayari baadhi ya timu za Ligi Kuu zimeanza kufanya usajili kwa ajili ya kuimarisha maeneo mbalimbali ndani ya vikosi vyao.
Miongoni mwa timu ambazo huenda hazikuwa na msimu mzuri kama ambavyo zenyewe zilitarajiwa ama kutarajiwa na mashabiki wao ni Yanga SC na Azam FC, ambazo sasa tayari zimeshafanya usajili wa baadhi ya wachezaji ili kuboresha timu zao.
Tayari Wana Jangwani Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hersi Said imeshakamilisha usajili wa Mabeki, Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union ambaye pia alikuwa anawaniwa na Wekundu wa Msimbazi Simba SC.
Pia Yanga wamekamilisha usajili wa Beki wa Klabu ya Polisi Tanzania, Yassin Mustapha ili kuboresha safu ya ulinzi hususan upande wa kushoto, ambapo sajili zote mbili zimefanyika leo Agosti 1, 2020. Hata hivyo, kabla ya usajili wa mabeki hao wawili, tayari Yanga jana Julai 31, 2020 ilikamilisha usajili wa Kiungo hodari wa timu ya Kagera Sugar, Zawadi Mauya ambaye aling'ara misimu kadhaa nyuma akiwa na timu ya Lipuli FC ya Iringa.
Beki wa timu ya Polisi Tanzania, Yassin Mustapha (kushoto) akisaini mkataba wa kuitumikia Yanga leo Agosti 1, 2020. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Eng. Hers Said
Kiungo Awesu Awesu (Kushoto) akitambulishwa juzi Julai 30, 2020 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kuwa mchezaji wa klabu hiyo baada ya kusajiliwa kutoka Kagera Sugar.
Kwa upande wa Matajiri wa Azam FC 'Wana Lamba lamba', nao hawako nyuma, kwani tayari wameshakamilisha usajili wa wachezaji wawili ambao ni Kiungo msumbufu, Awesu Awesu kutoka Kagera Sugar na kiungo Ally Niyonzima raia wa Rwanda kutoka klabu ya Rayon Sports ya nchini humo kwa mkataba wa miaka miwili.
Kiungo Ally Niyonzima raia wa Rwanda (Kulia) akisaini mkataba wa miaka miwili mbele ya Mtendaji Mkuu wa Azam Fc Abdulkarim Amin.
Niyonzima yumo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda Amavubi.
Kiungo Zawadi Mauya (Kati kati) akiwa na viongozi wa Yanga, Hersi Said ambaye ni makamu mwenyekiti kamati ya mashindano(Kushoto) na Kaimu Katibu wa klabu hiyo Patrick Simon (Kulia) wakati wa ukamilisho wa usajili.