DK. MAGUFULI: MIAKA 5 HAITOSHI, NIPIMENI KWA MIAKA 10



Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli akizungumza na wananchi kwenye uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga leo Septemba 3, 2020


Na Damian Masyenene –Shinyanga
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli leo Septemba 3, 2020 amefanya mkutano wa kampeni za kuomba kura katika mkoa wa Shinyanga pamoja na kuwanadi wagombea ubunge katika majimbo sita ya mkoa huo na madiwani.

Mkutano huo umefanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, ambapo pamoja na mambo mengi aliyoyaeleza kwa wafuasi, wanachama wa CCM na wananchi waliohudhuria uwanjani hapo, Dk. Magufuli amesema kwamba changamoto za nchi haziwezi kumalizwa kwa siku moja, hivyo hawezi kupimwa kwa miaka mitano pekee bali ameomba aongezewe muda mwingine ili apimwe utendaji wake kwa miaka 10.
 
Dk. Magufuli akiwasili katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga (Credit:Michuzi Blog)

Dk. Magufuli pia ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali itanunua ndege nyingine tano ikiwemo moja ya mizigo itakayokuwa inasafirisha bidhaa mbalimbali za wakulima na wafugaji kwenda nje ya nchi.

“Msinipime kwa miaka mitano, mnipime kwa miaka 10 ili mjue utendaji kazi wangu, katika miaka mitano iliyobaki tutafanya maajabu na naamini mtatupa tena miaka mingine mitano tutafanya mambo makubwa” amesema JPM.

Yaliyofanyika Shinyanga
Akieleza baadhi ya mambo aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano kwa mkoa wa Shinyanga, Dk. Magufuli amesema serikali imetumia jumla ya Sh Bilioni 31.9 katika miradi ya afya, ikiwemo kujenga hospitali ya mkoa wa Shinyanga ambayo imegharimu Sh Bilioni 3.6 mpaka sasa, hospitali za wilaya ya Kishapu na Shinyanga zilizogharimu Sh Bilioni 3.6, hospitali ya Msalala (Sh Milioni 634), vituo vya afya 11 (Sh Bilioni 4.2) na vituo vya afya 28 (Sh Bilioni 2.08).

Pia Sh Bilioni 29 zimetumika kwenye upande wa elimu hususani elimu bure, Sh Bilioni 60.8 katika miradi ya maji, hatua za awali za ujenzi wa reli ya kisasa ya Isaka-Shinyanga-Mwanza ambapo tenda zimeanza kutangazwa.

Atakayoifanyia Shinyanga
Akieleza baadhi ya mambo yaliyomo kwenye ilani ya chama chake ambayo yatafanyika kwa mkoa wa Shinyanga kwa miaka mitano ijayo, ni pamoja na kuimarisha vyama vya ushiriki, ujenzi wa maghala na vihenga vyenye uwezo wa kubeba tani zaidi ya 200,000, kujenga vituo vya kuchakata na kuhifadhi mazao ya kilimo ikiwemo Pamba, kuongeza Uzalishaji wa mazao yatokanayo na mifugo, kuhamasisha ufugaji wa samaki kwenye maeneo kame.

Pia ujenzi wa barabara ya Kolandoto-Lalago-Mwanuzi-Olabieni Junction, Mwanangwa –Misasi-Salawe- Kahama (Km 149), Solwa-Old Shinyanga (Km 65) na Kagongwa-Bukoba-Kahama zote kwa kiwango cha lami, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa ndege ili ndege ziweze kutua.

Vile vile, Kuimarisha mfumo wa kisera ili wananchi wanufaike na rasilimali za nchi ikiwemo upatikanaji wa teknolojia rahisi, mikopo, leseni na kutengewa maeneo ya kuchimba.

Changamoto

Dk. Magufuli ameeleza kuzitambua changamoto mbalimbali zinazousibu mkoa wa Shinyanga ikiwemo uhaba wa vifaa tiba na watumishi, malalamiko ya wachimbaji wa dhahabu Mwakitolyo, mkandarasi wa maji Solwa kutomaliza mradi kwa wakati, watumishi wa SHIRECU waliopunguzwa mwaka 2018 na wale waliopo kutolipwa stahiki zao, mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga kubadilisha umiliki wa vibanda katika soko kuu, stendi na soko la Kambarage bila kushirikisha wamiliki wa awali, na kilio cha kufufuliwa kiwanda cha Nyama Old Shinyanga kilichosimama tangu mwaka 2014.

Ambapo amewataka wahusika wakiwemo viongozi wa Serikali na wagombea ubunge, Patrobasi Katambi (Shinyanga Mjini) na Ahmed Salum(Solwa) kuyashughulikia. 

Katambi aomba chuo kikuu, soko
Awali akiomba kura zake kwa wananchi, Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobasi Katambi (CCM) alimuomba Dk. Magufuli kuuongezea mkoa wa Shinyanga taasisi ambazo zitaongeza mzunguka wa fedha katika jimbo hilo.

“Tunahitaji chuo kikuu katika mkoa wetu, tukipata walau soko moja kubwa na stendi mpya ya kisasa tutaondoa malalamiko ya wafanyabiashara,” amesema. 
 
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akizungumza na wananchi wakati akimkaribisha Mgombea Urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga

Wagombea ubunge katika majimbo sita ya mkoa wa Shinyanga na wa Viti Maalum wakiwa jukwaani na Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli wakiomba kura kwa wananchi

 Baadhi ya wafuasi wa chama cha CCM waliohudhuria kwenye uwanja wa Kambarage wakifuatilia sera kutoka kwa wagombea wao
 
 Maelfu ya wafuasi wa CCM na wananchi wakifuatilia mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga



 
  Wananchi na wana CCM waliojitokeza kwenye uwanja wa Kambarage wakifuatilia mkutano huo


 Picha na Marco Maduhu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464