Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta Jijini Dar es salaam.
Katika kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora, mbolea na viatilifu kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya milipuko.
Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Katika kufikia azma hiyo, Wizara ya kilimo imeanzisha Kitengo cha Masoko ya Mazao (Agricultural Marketing Unit) katika Idara ya Maendeleo ya Mazao inayosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia/kusimamia mifumo ya uuzaji wa mazao.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo Septemba 22, 2020 wakati wa uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta Jijini Dar es salaam.
Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma za Bima ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti Shughuli za Bima nchini (TIRA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), kampuni binafsi tano (5) za bima zimeanzisha Bima ya Mazao kwa lengo la kumsadia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupata dhamana ya mikopo.
Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali imefanya zoezi la kuwatambua, kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wakulima. Zoezi hilo lilifanywa kupitia Bodi za Mazao. Hadi sasa, wakulima 1,279,884 wa mazao ya biashara wamesajiliwa na kutengeneza kanzidata/database kwa lengo la kuwatambua na kusaidia katika utoaji wa huduma za kilimo ikiwemo huduma ya bima ya mazao.
Amesema kuwa Kilimo ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu kutokana na mchango wake katika uchumi. Takwimu zinaonyesha sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 28 katika Pato la Taifa, huku ikitoa ajira kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania.
Pia amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo vinavyoweka mkazo kwenye mapinduzi ya viwanda, kwa pamoja vanaitambua Sekta ya Kilimo kama mhimili imara utakaowezesha upatikanaji wa malighafi za viwanda na kukuza uchumi wa taifa letu.
Waziri Hasunga amesema kuwa Takwimu zinaonesha ni asilimia 8 ya mikopo yote iliyotolewa na taasisi za fedha katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilielekezwa katika sekta ya kilimo. Kiwango hicho kinajumuisha mikopo ya fedha pamoja na pembejeo za kilimo. Hiki ni kiwango kidogo ukilinganisha na umuhimu wa sekta hii katika uchumi wa taifa letu.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akiwasha trekta ishara ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta Jijini Dar es salaam.