JPM AKISTAAFU KUISHI KAGERA KARIBU NA VITEGA UCHUMI VYAKE

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli

RAIS John Magufuli ameweka wazi kwamba akistaafu utumishi wake wa urais, atakwenda kuishi mkoani Kagera, kwa kuwa anapapenda na ameweka vitega uchumi vyake ikiwemo mifugo.

Aidha, alisema yapo maneno kwamba fedha za misaada, zilizotolewa na wahisani mbalimbali kwa ajili ya athari za tetemeko la ardhi lililoikumba mkoa huo Septemba mwaka 2016 zimeliwa, sio za kweli, bali zilitumika kutekeleza miradi ya msingi mkoani humo ikiwemo ujenzi wa shule.

Aliyasema hayo jana mjini Bukoba mkoani Kagera, alipoomba kura kwa maelfu ya wananchi waliofika Uwanja wa Gymkhana kusikiliza sera za mgombea huyo wa Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Nimekuja hapa kwa ukumbusho mkubwa, hapa ndipo mahali  nilipewa warranty (hati) ya kusafiria kwenda kusoma Mkwawa High School…nimepanga baada ya kustaafu nitakaa Kagera na ndio maana nina ng’ombe wangu huku, ninapapenda, na watu wa Kagera ni wazuri wanahitaji maendeleo  na uchumi,” alisema Rais Magufuli aliyewahi kuwa Mbunge wa Biharamulo Mashariki mkoani Kagera.

Alisema mkoa huo anaupenda, ndio maana hata alipokuwa akitafuta Katibu Mkuu wa CCM, aliangalia maeneo mengi ya nchi na akamuona Dk Bashiru Ally ataweza, ndio maana alimchagua; na anatoka Kagera.

“Ninapapenda Kagera, hata nilipokuwa natafuta Katibu wa chama niliangalia wee nchi nzima, nikamuona Dk Bashiru ataweza, ametoka maisha ya chini, amefanya biashara ya ndizi pale Kemondo, ni mzalendo kati ya wachache wa kufuata miiko ya Mwalimu Julius Nyerere, ndio maana nikamteua awe Katibu Mkuu wa CCM,” alisema Rais Magufuli akimuelezea mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aliwaomba kura ya ndio wananchi, akiahidi kuendelea kuwatumikia kwa uaminifu iwapo watamchagua. Alisisitiza kuwa hataongeza hata siku moja baada ya kipindi hicho kumalizika.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464