JPM ALAANI MAUAJI YA KADA WA CCM NJOMBE



Na Amiri Kilagalila, Njombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. John Pombe Magufuli, ametuma salamu za pole pamoja na ubani wa shilingi milioni tano kwa familia ya Mlelwa, kufuatia mauaji na kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu (UVCCM) mkoa wa Iringa Ndugu Emmanuel Mlelwa.

Akitoa salamu za pole katika mazishi yaliyofanyika kijiji cha Luvuyo kata ya Madope wilayani Ludewa mkoani Njombe, Katibu wa NEC Uchumi na fedha wa Chama hicho ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Njombe, Dkt Frank Hawasi, amesema Rais Magufuli amesikitishwa na kifo cha kijana huyo kutokana na umuhimu wake kwa familia na taifa.

“Mwenyekiti wetu amepokea taarifa ya kifo cha kijana wetu Emmanuel Mlelwa kwa masikitiko makubwa sana,kwasababu sio kifo cha kawaida,lakini pia umuhimu wa kijana mwenyewe kwa nchi kwa ujumla,”amesema Dkt. Hawasi

Amesema Rais Magufuli amelaani kitendo hicho kwani hakikubaliki katika jamii “Mwenyekiti wa CCM Taifa analaani kitendo kilichofanyika kwa ndugu yetu Emmanuel Mlelwa kwasababu hakionyeshi utu,hakionyesho uzalendo na hakionyeshi utanzania wetu”aliongeza Dkt. Frank Hawasi

Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa kupitia kwa katibu wa NEC Uchumi na Fedha wa Chama hicho taifa Dkt. Frank Hawasi, ameagiza vyombo vya Dola mkoani Njombe kuwatafuta na kuwabaini waliohusika na mauaji ya kijana huyo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464