JPM: KATAMBI NI KIJANA NINAYEMPENDA, ATALETA MABADILIKO

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM, Patrobasi Katambi akiomba kura wakati wa mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga


Na Damian Masyenene –Shinyanga
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameonyesha imani yake kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia chama hicho, Patrobasi Katambi na kuwasihi wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanampitisha kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu ili alete mabadiliko yaliyokusudiwa.

Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Septemba 3, 2020 wakati akizungumza na wananchi, wanachama na wafuasi wa chama hicho kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na kuwanadi wagombea ubunge katika majimbo sita ya mkoa huo pamoja na madiwani.
  
Dk. John Magufuli akizungumza na wananchi kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati akiomba kura za urais

Akimzungumzia Katambi, Dk. Magufuli amesema Katambi ni kijana anayempenda, kumuamini na ni matumaini yake ataleta mabadiliko katika jimbo la Shinyanga Mjini, hivyo akawasihi wapiga kura kutosikiliza maneno ya pembeni bali wahakikishe wanamleta ili atumike.

“Wana Shinyanga Naomba mniletee Katambi, Naomba mniamini na mmuamini hatowaangusha….maneno maneno ya pembeni achaneni nayo, jana (Jumatano) nimekutana na Steven Masele naamini nitamtafutia kazi, zipo nyingi za kufanya,” amesema.

Katambi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadaye kujiengua na kwenda CCM kabla ya Rais Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, ambapo kwenye mchakato wa kutia nia aliutelekeza ukuu wa wilaya na kugombea jimbo la Shinyanga Mjini na kupitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu.

Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amempa maagizo ya kufuatilia na kuyafanyia kazi katika jimbo hilo pale atakapochaguliwa na wananchi kuwa Mbunge Oktoba 28, 2020.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha za mfuko wa barabara katika manispaa ya Shinyanga ambazo ameeleza kuwa zimekuwa zikitumika vibaya kila zinapoletwa na Serikali, huku pia akimtaka kumkumbusha kuhusu ujenzi wa barabara ya Neghezi –Ndala ambayo imekuwa ikisuasua.

“Kuna changamoto ya kutokamilika kwa barabara ya Ndala-Neghezi, Mkuu wa mkoa nataka viongozi wa Tarura na Tanaroads waanze kuandaa mpango kwa sababu fedha zipo zitatengwa na wewe Katambi hili liwe jambo lako la kwanza kunikumbusha ukichaguliwa, usije ukajisahau.

“Nataka Katambi utakapochaguliwa kitu cha kukifanyia kazi ni matumizi ya hovyo ya fedha za mfuko wa barabara zinazoletwa kwenye halmashauri yetu, nataka niwaahidi kwamba changamoto nimezisikia na zitashughulikiwa,” amesema Dk. Magufuli.
 
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Steven Masele (aliyevaa shati la CCM) akiwa pamoja na viongozi wa dini na serikali kwenye mkutano wa kampeni za Dk. Magufuli leo katika Uwanja wa Kambarage.
Picha na Marco Maduhu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464