Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake katika Kata ya Ngokolo leo Septemba 13, 2020.
Na Damian Masyenene, Shinyanga
LEO Septemba 13, 2020 Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi amezindua rasmi kampeni za kuomba kura na kunadi sera kwa wananchi wa jimbo hilo ili waweze kumchagua katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa Ngokolo Mitumbani katika Manispaa ya Shinyanga ukihudhuriwa pia na baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wa chama hicho kwenye kura za maoni akiwemo Steven Masele, na viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa pamoja na wagombea udiwani katika kata zote 17 za jimbo hilo.
Akiomba kura kwa wananchi na kunadi sera zake, Katambi amesema jimbo hilo lenye takribani watu 191,000 lazima libadilike kimaendeleo na kuwataka wananchi kutofanya mzaha wakati wa kufanya maamuzi ya kupiga kura, bali wamchague yeye aweze kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli.
Katambi alieleza kwamba endapo atachaguliwa basi atahakikisha anafanikisha kuongezwa kwa vituo vya afya walau kila kata akianza na Kata ya Ngokolo ambayo haina zkituo cha afya kwa sasa, ambapo lengo ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, vile vile ameahidi kuboresha huduma za kliniki kwa mama na mtoto kwa kusimamia mikataba ya halmashauri kuhusu lishe kwa watoto na akina mama wajawazito.
Ameongeza kwa kubainisha kwamba licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara mkoa wa Shinyanga, bado mzunguko wa fedha katika mkoa huo ni mdogo, hivyo atasaidia upatikanaji wa tafiti zitakazoonyesha fursa za uwekezaji na kukuza sekta ya viwanda ili kuongeza mzunguko wa fedha katika jimbo hilo.
"Mkinipa ridhaa pamoja na madiwani na Rais tunahitaji kufanya utafiti wa kuongeza mazao mengine ya biashara yatakayosaidia kuongeza pato na mzunguko wa fedha katika mkoa wetu.
"Pia tutatoa hamasa ya kuwa na taasisi zingine za kutoa huduma za kijamii, tunahitaji walau vyuo vikuu wivili lazima kuwe na mwingiliano wa watu kutoka na kuingia....tunaenda kuweka taasisi ya kufanya utafiti juu ya fursa zilizopo na kutengeneza mwongozo wa uwekezaji ili kuainisha fursa zilizopo na kukuza uchumi," amesema.
Katambi amesindikizwa na wagombea ubunge wa Viti Maalum katika mkoa huo, Lucy Mayenga, Dk. Christian Mzava na Santiel Kirumba ambao wamewasihi wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwashawishi wananchi kuipigia kura CCM na kumchagua Rais Dk. John Magufuli, Mbunge Patrobas Katambi na madiwani wote wa chama hicho.
Awali akiomba kura za udiwani kwa wananchi wa kata ya Ngokolo, Mgombea udiwani wa kata hiyo, Victor Mkwizu ameahidi kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anatatua kero za wananchi katika mitaa yote saba ya kata hiyo kupitia mikutano ya kuongea nao na kuainisha kero hizo na kuzitafutia ufumbuzi.
Vile vile, ameeleza kuwa katika vipaumbele vyako, mojawapo ni kushughulikia changamoto ya huduma ya afya katika kata hiyo kwa kuhakikisha wanapata kituo cha afya ili kuosogeza karibu huduma hiyo kwa wananchi.
"Zipo changamoto katika mikopo ya akina mama, vijana na walemavu, kwenye viwanja, miundombinu ya barabara, elimu na michezo, naomba mnichague kuwa diwani tuweze kushikamana kuzitatua kero hizo katika kata yetu," amesema.
Patrobas Katambi akinadi sera na kuomba kura za ubunge kwa wananchi katika uwanja wa Ngokolo Mitumbani Manispaa ya Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde & Marco Maduhu
Mgombea ubunge viti maalum mkoa wa Shinyanga, Dk. Christina Mzava akipiga magoti kumuombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (kulia)
Baadhi ya waliotia nia ya ubunge jimbo la Shinyanga Mjini wakiongozwa na MNEC, Gasper Kileo (aliyeshika kipaza sauti) ambaye pia Meneja Kampeni wa Patrobasi Katambi wakimuombea kura kwa wananchi
Patrobas Katambi akizungumza na wananchi katika uwanja wa Ngokolo manispaa ya Shinyanga
Wagombea udiwani katika kata 17 za jimbo la Shinyanga wakiwa mbele katika mkutano huo ili wananchi wawaone
Katambi akiendelea kunadi sera zake kwa wananchi
Viongozi na makada mbalimbali wa chama wakifuatilia mkutano huo
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam akizungumza kwenye mkutano huo
Mgombea ubunge Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba (kushoto) akizungumza na wananchi
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa (kushoto) akimnadi mgombe udiwani Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu
Baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na makada akiwemo Gaspel Kileo na Steven Masele wakifuatilia mkutano huo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akiwanadi wagombea ubunge viti maalum na mgombe ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi
Viongozi wa Chama mkoa, baadhi ya wagombea ubunge viti Maalum na Patrobas Katambi wakifanya dua kabla ya kuanza kwa zoezi la kunadi sera mbele ya wananchi
Picha zot na Kadama Malunde na Marco Maduhu