KHERI JAMES, BUTONDO WAAHIDI KUMALIZA MIGOGORO YA WACHIMBAJI WADOGO KISHAPU



 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James (kulia) akimnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu mkoa wa Shinyanga kupitia CCM, Boniface Butondo (kushoto) katika mkutano wake kata ya Mwadui wilayani Kishapu
 
Na Suzy Luhende -Kishapu
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James amewataka wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka migodi ya wawekezaji ya Williamson Diamond Ltd na Al-Hilary Minerals kuiamini CCM kwa kukipigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Kheri ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alisema chama chake tayari kimepitia kwa kina mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi ambao wengi wao shughuli yao kubwa ni wachimbaji wadogo na wamiliki wa migodi hiyo.

Akiwa katika ziara yake, katika kata ya Mwadui Luhumbo wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga, Kheri alisema serikali kupitia wataalamu wake wa wizara ya madini wamepitia utaratibu wa umiliki wa ardhi kati ya wachimbaji hao wadogo na migodi na kubaini kuwepo kasoro ambazo iwapo watakipigia kura chama cha mapinduzi kitaanza kushughulikia mgogoro huo.

Alisema kuwepo na maneno ya baadhi ya wagombe wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakipotosha jamii kuhusiana na mgogoro huo hali ambayo Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ziara mkoani shinyanga katika kata ya magonzo aliahidi kuutanzua mgogoro kupitia watendaji wake.

Dkt. Magufuli aliwataka wananchi kukipa chama cha mapinduzi ridhaa kwenye nafasi zote ikiwemo ya ubunge ambapo mgombe ubunge jimbo la Kishapu, Boniface Butondo alipewa kazi yake ya kwanza itakuwa ni kushughulika na mgogoro huo.

Katika mkutano huo, Mgombea ubunge huyo kwa tiketi ya CCM, Boniface Butondo akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo ya Mwadui Luhumbo alisema tayari ameshapewa mahala pa kuanzia pindi atakapochagulia na kuapishwa kama mbunge wa jimbo hilo la Kishapu.

Mheshimiwa Magufuli ameshanipa maelekezo ya namna ya kulishughulia suala hilo pindi mtakaponichagua na kuwa mbunge wa kishapu ambapo nitaenda kuonana na wataalam wa sekta ya madini ili tushirikiane kutatua mgogoro kwa manufaa ya wachimbaji wetu wadogo ambao hawajanufaika ipasavyo na madini ya Almasi,” alisema Butondo.


Katika hatua nyingine Butondo alisema akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu anafahamu kuwa serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta za miundombinu, Maji, elimu na Afya.


Hivyo alisema kazi aliyonayo mbele pindi atakapopewa Ridhaa na wananchi ni kuhakikisha fedha hizo zinafanyakazi kwa manufaa ya wananchi wa jimbo la Kishapu.


Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata ya Mwadui Luhumbo kupitia CCM, Francis Manyanda alisema kwa kushirikiana na Mbunge watahakikisha wanasimamia shughuli za maendeleo ikiwemo kuwatetea wachimbaji wadogo wa almasi wanaoishi pembezoni mwa migodi hiyo.

TAZAMA PICHA
Mwenyekiti wa Umoja wa vijana UVCCM Taifa James Kheri akizungumza na wananchi wa Mwadui Luhumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ambapo aliwaomba wachague wagombea wa chama cha mapinduzi kwa ajili ya kuondoa migogoro na kuleta maendeleo.
 
 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwadui Luhumbo
 
 Wafuasi wa CCM wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James
 
Boniface Butondo akinadi sera zake kwa wananchi wa kata ya Mwadui Luhumbo wilayani Kishapu kwenye mkutano wa hadhara wa mwenyekiti wa UVCCM Taifa, James Kheri.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464