Dk. Harrison Mwakyembe
MKAKATI wa mgombea ubunge jimbo la Kyela kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Mlaghila, wa kuendelea kujinadi kwenye mikutano ya kampeni bila kuzungumzia miradi iliyotekelezwa na mtangulizi wake, umeanza kukipa faida Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Baadhi ya viongozi, wanachama wa CCM na wananchi wengine waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema mkakati huo unakiondolea chama tawala mtaji na msingi muhimu wa kura.
Walisema hatua hiyo inainufaisha CHADEMA ambayo inaielezea miradi yote kwa ufasaha na kuahidi kuiendeleza huku pia ikibainisha changamoto zilizoko jimboni humu.
Kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa na mbunge aliyemaliza muda wake, Dk. Harrison Mwakyembe, pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, mgombea ubunge wa CHADEMA, Alinanuswe Mwalwage, ameonyesha kuwa kivutio kwa wapigakura.
Katika kampeni zake, Mwalwage amekuwa akikiri kuwa maendeleo hayana chama, hivyo kupongeza kazi iliyofanywa na serikali ya CCM na kuelezea baadhi ya kasoro na kuahidi kuyafanyia kazi.
Hatua hiyo inawafanya baadhi ya wananchi wanaamini kuwa mgombea huyo wa CCM ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Kyela, bado anasumbuliwa na mivutano iliyojitokeza kwenye kura za maoni pamoja na kwamba watiania wenzake 39 wametamka hadharani kuwa wanamuunga mkono.
Mlaghila ambaye vikao vya juu vya CCM vilirejesha jina lake kuwania ubunge Kyela, hamtaji kabisa mtangulizi wake wala miradi iliyofanikishwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kuwaachia CHADEMA uwanja mpana wa kisiasa kujimwaga.
Alidhihirisha hivyo hata siku ya uzinduzi wa kampeni zilizofanyika mjini hapa Septemba 11, mwaka huu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula.
Katika uzinduzi huo, Mlaghila hakutaja kabisa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye jimbo hilo miaka mitano iliyopita au kabla.
Akitumia kauli ya Rais Magufuli ya maendeleo hayana chama, mgombea wa CHADEMA, Mwalwage, anaitaja miradi mikubwa iliyotekelezwa kipindi cha nyuma na kusema inaendana na matarajio yake na chama chake katika kutatua kero za wananchi.
Miradi mikubwa iliyotekelezwa kipindi cha nyumba ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Kikusya - Matema (km 39.5), ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha mpakani na Malawi (Kasumulo) na ujenzi wa chelezo katika bandari ya Itungi.
Mingine ni ujenzi wa meli tatu katika Ziwa Nyasa, mradi wa maji wa Kapapa wa unaohudumia wananchi 13,500; Kituo cha Afya cha Ipinda, ukarabati mkubwa Hospitali ya Wilaya na ujenzi wa vituo vya afya vikiwamo vya Njisi na Kilasilo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464