Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk.John Magufuli
WANANCHI wameonywa kutokukubali kuingia kwenye mtego wa kugawa nchi kiutawala kwa mfumo wa majimbo, kwani yana madhara na kuleta mgawanyiko mkubwa, ukiwemo wa ukabila na mwisho kuvuruga amani na kuifarakanisha nchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana katika maeneo tofauti mkoani Tabora na Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli.
Alisema hayo wakati akiomba kura kwa wananchi wa maeneo hayo sambamba na kuwaombea wagombea wengine wa udiwani na ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Akizungumza na wananchi hao, mgombea huyo aliwaonya na kuwataka wananchi kuwa makini na wagombea urais wa vyama vingine vya siasa, ambao wanajinadi kwa sera ya kugawa nchi kwenye utawala wa majimbo.
Alisema kuwa huo ni mtego wa kugawa nchi na kuleta mfarakano. “Tusipokuwa na amani suala la utulivu uliopo litaondoka, hatutaweza kwenda mashambani kulima, hatutaenda kanisani au msikitini, kwa ujumla maisha yatakuwa magumu sana hata masuala ya ujenzi wa viwanda haitawezekana…waulizeni wakimbizi waliopo hapa ambao wengine wameshakuwa Watanzania walikimbia amani kwao, tusifanye makosa, tutajuta,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza katika mikutano hiyo Urambo na Tabora Mjini jana, Rais Magufuli alisema wagombea hao wa vyama vingine, wanasema kwenye kampeni kwamba nchi itagawanywa kwenye utawala wa majimbo na kusema wakishatengeneza majimbo hayo ni kutengeneza mgawanyiko mkubwa.
Alisema Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliuona na kukataa mfumo huo, ambao kama ungetekelezwa, nchi isingekuwepo hapa ilipo.
“Mwalimu Nyerere alituweka pamoja makabila yetu zaidi ya 120, hakutaka mfumo wa majimbo ya ukanda kwa sababu kufanya hivyo ni kutekeleza matakwa ya wanaotaka kuja kututawala na kupora rasilimali zetu baada ya sisi kuingia mtegoni na nchi kuchafuka, hayo mambo ndio wanafundishwa huku nje, tusikubali kuifarakanisha nchi kamwe,” alisisitiza Rais Magufuli anayeomba kipindi cha pili cha uongozi wa nchi.
Alisema Tanzania imeshapiga hatua kubwa ya maendeleo na kama ikikubali kuingia kwenye mifumo ya ovyo, itakuwa ni kuirudisha nyuma.
Alibainisha kwamba hata nchi zilizojaribu kuiga mfumo huo, zimevurugika na jambo hilo halitaki litokee nchini.
“Hivi tungekubali mfumo huo, je, leo fedha za ujenzi wa barabara za kuunganisha Kigoma na mikoa mingine shilingi bilioni 567 zingetoka wapi? Tabora tumeleta maji kutoka Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 600, je, Tabora wangezitoa wapi? Maana hazikutolewa na maeneo hayo tu, bali ni michango ya nchi nzima, kataeni mbinu za kutugawa, zikataeni kwa nguvu zote” alisisitiza Rais Magufuli.