KILA binadamu ataonja umauti! Hili halina mjadala. Lakini, umeshawahi kujiuliza 'kwanini watu wengi taarifa za misiba yao hubainisha wamefariki dunia usiku?' Ni swali la kawaida katika udadisi wa kibinadamu.
Katika kufuatilia matangazo ya vifo, bila shaka utakubaliana na mimi kwamba, mengi huwa na taarifa kuwa "...amefariki dunia usiku wa kuamkia leo", haijalishi amefia nyumbani au hospitalini.
Udadisi huu unaweza kuibua hisia ya mambo mengi ambayo kiuhalisia pengine hayahusiani kabisa na sababu za watu wengi kufariki dunia nyakati za usiku.
Zipo dhana na hadithi nyingi za mapokeo juu ya masuala ya imani za kishirikiana zinazosimuliwa katika jamii zetu za Kiafrika; Hadithi za simulizi za mambo ya wachawi wanaoroga na kuua watu usiku.
Hilo nalo pengine likakusukuma kuamini kuwa huenda watu hao hufa kwa kurogwa.
Katika kufuatilia ukweli wa hisia hizo kwamba huenda watu wanaofariki dunia usiku ni kutokana na dhana hiyo ya kuwapo kwa uchawi, mwaka 2011 nilimwuliza aliyekuwa Mnajimu Mashuhuri Afrika Mashariki, Sheik Yahya (marehemu) "kwanini watu wengi hufa usiku?"
Pengine kwa sababu ilikuwa ni asubuhi, swali langu lilionekana kumkera Sheikh Yahya niliyekutana naye katika ofisi zake, Magomeni, alinifokea na kuniuliza "wewe unataka wafe saa ngapi?", kisha akanitimua ofisini kwake.
Baada ya saa kadhaa kupita, Sheikh Yahya alitulia na kuniita ofisini kwake, akaniambia: "Sasa rafiki yangu, asubuhi yote unaleta mambo ya vifo?"
Baada ya hapo, akaniambia kwamba, kwa elimu ya unajimu, hana jibu la swali hilo, akidai kuwa kifo hutokea tu muda wa uhai wa mtu duniani unapokwisha.
Ukiachana na imani za kishirikiana, ipo dhana nyingine ya imani za kidini kuhusu sababu za vifo kwa mwanadamu.
Katika mafunzo ya imani za kidini, waumini hufundishwa kwamba mwisho wa uhai wa mwanadamu hapa duniani ni kufa, ingawa imani hizo hazitaji sababu wala muda wa mwanadamu kufa.
Tunaaminishwa kwamba wote tutakufa na kila mmoja na kifo chake na sababu zake za kifo.
Hili la mtazamo wa sababu za imani za kiroho linaonekana kukubaliwa na watu wengi niliozungumza nao katika udadisi wangu, lakini sikupata sababu mahususi "kwanini watu wengi hufa usiku?".
Kwa mfano, nilipomwuliza imamu wa msikiti mmoja jijini Dar es Salaam juu ya suala hilo, maelezo yake hayakutoa jibu la sababu za moja kwa moja, akisema: "Mwenyezi Mungu ndiye anapanga mwanadamu aishi kwa muda gani, azaliwe saa ngapi na afe saa ngapi.
"Katika mafundisho ya Uislamu, Bwana Mtume anatuambia kulala ni sawa na kufa. Mtu anapolala usiku ni kama amekufa, hayupo tena katika maisha ya kawaida. Na ndiyo maana tunapoamka tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufufua baada ya umauti, yaani usingizi."
Vilevile, Mchungaji Noah Kiyondo anaunga mkono mtazamo huo kwamba kifo kinapangwa na Mungu akifafanua: "Uhai wa mwanadamu upo chini ya mamlaka ya Bwana, yeye ndiye mwenye kutupa uhai na maisha ya dunia kwa nyakati zake.
"Suala la kufa usiku, asubuhi, machana au jioni siyo kitu mbele za Bwana, muhimu ni mwanadamu kujiandaa kwa umauti maana yaja kama mwizi aibavyo," anasema.
Ukiachana na dhana hizo za mila na imani za kidini, kuna mtazamo wa kisayansi, hasa unaohusiana na masuala ya tiba na afya ya mwanadamu.
Dk. Festo Maduhu anayefanya kazi katika moja ya hospitali za taasisi binafsi jijini Dar es Salaam, anabainisha kile anachokiamini kisayansi vifo vingi kutokea nyakati za usiku.
Tabibu hiyo anasema katika mtazamo wa kisayansi, vifo vingi vya usiku vinatokea kwa sababu ya mabadiliko katika mfumo wa hali ya hewa kuu mbili zinazotawala mazingira ya viumbe hai ambazo ni Oksijeni na Kabonidaioksaidi.
Dk. Maduhu anasema: "Wanadamu tunaishi kwa kutegemea hewa ya Oksijeni. Hewa hii ndiyo tunayoivuta na kuingiza ndani ya miili yetu kwa kupitia pua, kisha inaingia kwenye mapafu yetu na kwenda kwenye viungo vingine vya miili yetu kuvipa uwezo wa kufanya kazi ya kuendesha uhai wetu.
"Na wakati unapovuta hewa hiyo, ndani ya miili yetu hutoka hewa ya Kaboni (Kabonidaioksaidi) ambayo tunaiita hewa chafu. Ni hewa hatari kwa maisha yetu.
"Lakini, hii Oksijeni tunayotumia nayo hutengenezwa na mimea ambayo ni miti na majani, ambayo nayo huishi kwa kuvuta hewa ya Kaboni mchana kutwa na inapofika usiku, hubadilika na kuanza kuvuta hewa ya Oksijeni kwa wingi wakati sisi binadamu bado tunaendelea kuvuta hewa ileile ya Oksijeni.
"Kwa maana hiyo, nyakati usiku kunakuwa na upungufu wa hewa hiyo (Oksijeni) kwa sababu binadamu na mimea, wote tunatumia hewa moja."
Katika hali hiyo, Dk. Maduhu anasema ni rahisi sana kwa wagonjwa au watu wenye matatizo ya kupumua vizuri kufariki dunia nyakati hizo za usiku.
Anabainisha kuwa watu wanaoishi kwenye nyumba zilizo karibu na miti au majani ambayo yana hali ya kijani kibichi kwa nyakati au maua ya nyumbani, wana hatari kukabiliwa na upungufu wa Oksijeni kwenye maeneo yao.
"Hii ndiyo sababu kubwa kisayansi watu kufa usiku. Ni vizuri watu wakapanda miti hatua kadhaa mbali na nyumba zao hasa maeneo ya madirisha na kuepuka pia kupanda haya maua yenye majani yenye kijani kibichi na asili ya uteketeke kwenye madirisha au ndani ya sebule zao," anaonya.
Mtazamo huo wa Dk. Maduhu unaungwa mkono na Daktari Bingwa wa Usingizi na Mfumo wa Neva, Dk. Brandon Peters, ambaye katika chapisho lake la Mei 8 mwaka huu alilolipa jina la 'Why Do People Die in Their Sleep?' (Kwanini Watu Hufariki Dunia Usingizini?), anaanika sababu tisa za vifo vya usingizini.
Miongoni mwa visababishi vya vifo hivyo vilivyotajwa na Dk. Peters, ni shambulio la moyo kutokana na mwili kupokea kiwango kidogo cha Oksijeni wakati wa mtu akiwa usingizini pamoja na majanga (mfano tetemeko la ardhi), sumu mwilini na matumizi ya dawa za kulevya.